Ile shoo kubwa na ya kijanja iliyokuwa ikisubiriwa na mashabiki wengi wa burudani imewadia ambapo leo Aprili, 5 (Sikukuu ya Pasaka) ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar mastaa wa muziki Bongo kama, Ali Kiba ‘Mwana Dar Live’, Isha Mashauzi, Msaga Sumu na wengineo wanatarajiwa kutikisa vilivyo mashabiki watakaojitokeza.
Kwa mujibu wa Mratibu wa burudani katika ukumbi huo, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ aliawaomba mashabiki wote kufika kwa wingi kujionea mastaa hao wakifanya maajabu jukwaani.
“Moto wa burudani utawaka ndani ya Dar Live Pasaka hii. hivyo niwaombe tena, siku hii si ya kukosa kutokana na burudani tulizowaandalia,” alieleza Abby Cool.
Ali Kiba akiwa katika moja ya shoo yake aliyopiga Dar Live miaka ya nyuma (Picha ya Maktaba ya Global Publisher)
ALI KIBA
Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2013, Ali Kiba hajafanya shoo yoyote katika ukumbi huo na kwa mara nyingine anakuja kama Mwana Dar Live kutokana na wimbo wake unaotikisa kwa sasa wa Mwana.
“Kwa mara ya kwanza Dar Live, Ali Kiba ataimba nyimbo zake live kwa kutumia vyombo na hii itakuwa mwanzo mwisho hivyo itakuwa burudani ya aina yake.
“Kikubwa kitakachoamsha shangwe kwa mashabiki ni staili yake mpya atakayoizindua ya Chekecha Cheketua inayotokana na wimbo wake wenye jina hilohilo huku akiwa na madensa wake wapya.”
Pia mashabiki watapata kuonjeshwa ngoma zinazobamba alizofanya na mdogo wake wakiwa kama Kiba Square ambazo ni Kidela, Pita Mbele na nyingine nyingi.
Isha Mashauzi akiwaburudisha wadau wa muziki ndani ya Dar Live katika moja ya shoo zake za nyuma (Picha ya Maktaba ya Global Publisher).
ISHA MASHAUZI
Kiongozi wa kundi la muziki wa Pwani, Mashauzi Classic, Isha Mashauzi ‘Jike la Simba’ naye atakuwepo leo kutoa burudani mashabiki wote wa muziki huo. “Kwa mara ya kwanza Isha atautambulisha wimbo wake wa Nimpe Nani huku Mashauzi Classic wakiwakonga kwa nyimbo zao kali kama Ropokeni Yanawahusu , Ni Mapenzi Tu, Tupendane, Bonge la Bwana na nyingine nyingi.”
Mashauzi pia watatoa sapraizi kubwa ikiwa ni pamoja na kuachia nyimbo zao tatu kwa mpigo ambazo ni Tuacheni Tulale, Mapenzi Yamenivuruga pamoja na Wema Hauwezi.
PAM D
Burudani pia itafunikwa na msanii anayekuja kwa kasi, Pamela Daffa ‘Pam D’ ambapo atapiga shoo ya aina yake akiwa sambamba na madensa wake. Pam D atawabamba na ngoma yake ya Nimempata aliyoshirikiana na Mesen Selekta ambayo ni habari ya mjini kwa sasa.
MASAI WARRIORS
Mapema kuanzia asubuhi hadi jioni kutakuwa na kundi maarufu la Masai Warriors ambalo litatoa burudani kibao kwa watoto kama vile kucheza na magunia, sarakasi, yoga, kuimba, kugawa zawadi na vingine vingi.
“Niwaombe tu wazazi wawaruhusu watoto wao kuja sehemu hii muhimu kwa burudani za kijanja. Tumewaandalia pia michezo mingi kama vile ya kubembea, kuteleza,kuogelea na kila mmoja atahakikisha anarudi na zawadi nyumbani kemkemu,” alisema Abby.
MSAGA SUMU
Pazia la burudani kwa watu wakubwa litafunguliwa usiku ambapo kwa watu wote watakaofika mapema watapata fursa ya kupiga picha ‘red carpet’ na mastaa wote watakaofika leo sambamba na kuongea nao machache.
“Kwa mara ya kwanza atazindua nyimbo zake tatu kwa mpigo ambazo ni Marafiki Gani, Shemeji Unanitega pamoja na Kidole Changu.”
Mtandao huu unawatakia kila lakheri wakristo wote Duniani katika kusheherekea sikukuu hii ya Pasaka leo.