Ndugu zangu,
Nimepokea kwa masikitiko habari za kifo cha ghafla cha msanii mhamasishaji John Komba.
Nilikuwa kijana mdogo sana nilipomwona kwa mara ya kwanza John Komba akitumbuiza ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa mwaka 1981.
Nilimwona John Komba na kikundi chake cha Kwaya ya JKT Mgulani. Alikuwa kijana mwembamba. Alikuwa mwanzoni kabisa mwa nyota yake kuanza kung’aa kuwarithi wasanii wahamasishaji wa tangu enzi za TANU, akina Mzee Makongoro na Chalamila.
Hata kwa masikio ya utotoni, nilimwona John Komba mwenye nyota itakayong’aa zaidi. Tungo zake zilivutia, sauti yake pia.
Bila shaka, John Komba ni msanii aliyekisaidia sana Chama Cha Mapinduzi katika kueneza jumbe zake.
Mfano, miaka ile ya 80, CCM, kwenye moja ya mikutano mikuu ya CCM, vijana waliombwa na chama chao kujitokeza kwenye kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi za wilayani.
Ni John Komba aliyeufikisha ujumbe huo vema kabisa kwa tungo ambayo bado naikumbuka, aliimba:
” Vijana wanaombwa, waende wilayani, kwenye vikao vya chama vya utendaji wilaya”.
Kwa bara la Afrika, ilipata kutokea, miaka ile ya 80, kwa kikao cha OAU kuvunjika. John Komba akaimba kwa masikitiko:
” Haijatokea hata siku moja, kikao OAU kikaja vunjika!” kisha kuziasa nchi kuendelea kiimarisha OAU.
Hakika, kuna wa kizazi changu, ambao tumekua tukizisikiliza, kuhamasika na kujifunza kwa tungo za John Komba.
Tutakukumbuka, John Komba.
Maggid Mjengwa,
Iringa.