Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (Mb), akiwasili Bungeni Mjini Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka 2014/15 leo.
Na MOblog Team, Dodoma
BAJETI mpya ya mwaka wa fedha ya 2014/2015 iliyopitishwa leo na Bunge la Bajeti mjini Dodoma, imeendelea kuwa chungu kwa watumiaji wa vinywaji mbalimbali nchini.
Baada ya serikali kuendelea kupandisha ushuru wa bidhaa za vinywaji baridi, vilevi pamoja na bidhaa za tumbaku kwa kila bidhaa moja.
Akizungumza wakati akitaja mabadiliko hayo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya, amesema ushuru wa vinywaji baridi, umepanda kutoka shilingi 91 hadi shilingi 100 ikiwa ni ongezeko la shilingi 9 kwa lita.
Amesema bidhaa za maji ya matunda (Juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini, imepanda kutoka shilingi 9 hadi shilingi 10 , ikiwa ni ongezeko la shilingi moja kwa lita.
“Pia ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 110 hadi shilingi 121, ambayo ni sawa na ongezeko la shilingi 11 kwa lita.
“Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini isiyo oteshwa, ikiwemo kibuku, zimepanda kutoka shilingi 341 hadi shilingi 375, ikiwa ni ongezeko la shilingi 34 kwa lita,”amesema Mkuya.
Amesema ushuru wa aina nyingine za vilevi (bia) nazo zimepanda kutoka shilingi 578 kwa lita hadi shilingi 635 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 57 kwa lita.
Vilevi hivyo ni pamoja na Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, ambayo ushuru wake umepanda kutoka shilingi 160 hadi shilingi 176 ikiwa ni ongezeko la shilingi 16 kwa lita.
“Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka shilingi 1,775 imeongezeka hadi shilingi 1,953 ikiwa ni ongezeko la shilingi 178 kwa lita.
”Ushuru wa vinywaji vikali umepanda kutoka shilingi 2,631 kwa lita hadi shilingi 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 263 kwa lita,”amesema Mkuya.
Aliongeza kuwa licha ya ongezeko hilo katika bidhaa za vimiminika lakini, ushuru wa bidhaa za maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka.
Wakati huohuo, Waziri Mkuya amesema kuwa serikali imefanya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Bidhaa kwenye Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini.
Iliyopanda kwa kiwango cha asilimia 75 na kuongezeka kutoka shilingi 9,031 hadi kufikia shilingi 11,289 kwa sigara elfu moja, ambayo ni sawa na ongezeko la shilingi 2,258 kwa sigara elfu moja na shilingi 2.25 kwa sigara moja.
Amesema bei ya Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango hicho angalau asilimia 75, imepanda kutoka shilingi 21,351 hadi shilingi 26,689 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 5,338 na shilingi 5.30 kwa sigara moja.
”Hata hivyo Sigara nyingine zenye sifa tofauti na hizo zimepanda kutoka shilingi 38,628 hadi kufikia shilingi 48,285 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 9,657 sawa na shilingi 9.65 kwa kila sigara moja.
”Pia tumbaku iliyo tayari kutengeneza sigara (cut filler) nayo imepanda kutoka shilingi 19,510 hadi shilingi 24,388 ikiwa ni ongezeko la shilingi 4,87 kwa kilo,”amesema Mkuya.
Amesema licha ya mabadiliko ya bei hizo bado ushuru wa “sigara” unabaki kuwa asilimia 30 na kwamba mabadiliko hayo yanatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 124,292.0.