Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Waislamu nchini watakiwa kutumia kipindi cha mfungo kutoa sadaka, kuwahudumia watoto yatima, wagonjwa na watu wasiojiweza.

$
0
0

IMG_7532

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa nasaha zake alipowafuturisha viongozi wa dini mbalimbali mkoani Lindi.

Waislamu nchini wametakiwa kutumia kipindi cha mfungo wa Ramadhani kuomba na kutubu dhambi zao pia kuwasaidia watu wasiojiweza ili wapate thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha viongozi wa dini mbalimbali mkoani Lindi.

Mama Kikwete amesema kuwa kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani ni kipindi cha kuomba na kutubu dhambi ili yule aliyefunga aweze kujiunganisha na Mwenyezi Mungu.

Amesema “Ibada na maombi yenu viendane na kutoa sadaka, wahudumieni watoto yatima, wagonjwa na watu wasiojiweza, muwe watu wa upendo kwani mahali penye upendo hakuna chuki, vita wala mafarakano”.

Ameendelea kusema kuwa kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kufuturu kwa pamoja na viongozi wa dini mbalimbali na kuwaombea  kwa Mwenyezi Mungu awajalie funga ya heri na  kuwazidishia huruma, upendo na mshikamano ndani ya mioyo yao.

Mama Kikwete pia amewataka viongozi hao wa dini kuhubiri amani kwa waumini wao na kuhakikisha kuwa hawaipotezi  amani kwa mambo yasiyo na tija, kwani kuna nchi waliichezea amani na hivi sasa wanaishi kwa hofu na maisha ya vita.

Mama Kikwete amesisitiza “Mjitahidi kila mnapokuwa katika maeneo yenu ya ibada, sherehe na katika huzuni muhubiri juu ya kuwepo kwa  amani kwani pamoja na umaskini wetu, Tanzania tumejaliwa kuwa na amani, kwani kuna nchi ambazo ni  matajiri lakini hawana amani na wananchi wake wanaishi maisha ya mashaka na hofu”.

Kwa upande wake Shekhe na Kadhi Mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani amemshukuru Mama Kikwete kwa ajili ya futari aliyoiandaa kwa ajili yao na  kusema kuwa kufunga ni moja kati ya  nguzo tano za dini ya Kiislamu na hiyo ni nguzo ya nne.

Shekhe Mushangani amesema “Amri ya kufunga iliyotolewa na Mtume Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W) akiwa Madina mwaka wa pili, ndipo ilipoteremka amri hii hivyo basi waislamu wenye afya njema wanatakiwa kufunga”.

Ameendelea kusema kuwa mtu anayefunga na kuwa na  hali ya kuamini na kutarajia thawabu anasamehewa makosa ya mwaka wote uliopita nyuma na mfungo mosi anaanza upya kuhesabiwa dhambi zake.

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles