Mjumbe wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, George Lubeleje ( wa tatu kulia).Picha na Maktaba.
Na Mwandishi wetu
Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa inatarajia kuanzisha Benki ya maendeleo ya Serikali za Mitaa ambayo pamoja na mambo mengine Jukumu lake la Msingi litakuwa ni Kutoa Mikopo yenye masharti nafuu kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi inayolenga kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na Mapato ya Halmashauri ili kujiletea Maendeleo ndani ya Halmashauri na watumishi wake.
Hayo yalielezwa leo na Mjumbe wa Bodi hiyo George Lubeleje alipoongea na Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Mji-Kibaha kwenye ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Lubeleje alisema kuwa Bodi ya Mikopo kwa hivi sasa imeongezewa jukumu la kutoa dhamana kwa Serikali za Mitaa ili ziweze kupata Mikopo kwenye mabenki ili ziweze kujenga na kukarabati Miundombinu na kutoa huduma za msingi kwa kuchochea shughuli za kiuchumi. Aidha, Lubeleje aliyeliongoza Jimbo la Mpwapwa akiwa Mbunge kwa Miaka 20 alisema anatambua kuwa kila Halmashauri ina vipaumbele vyake vinavyoendana na Mazingira na hivyo huhitaji njia za ziada za kupata mapato yake.
Akizungumzia Masharti na Vigezo vya Halmashauri kupata Mkopo, Lubeleje alisema kuwa Sharti la Msingi ni Halmashauri Kuchangia mchango wake wa akiba. Aidha, aliongeza kuwa Bodi imeweka masharti na vigezo vinavyotakiwa vitimizwe ambavyo ni Baraza la madiwani kukaa kikao rasmi na kuazimia kukopa, Kuwepo na uthibitisho wa usimamizi mzuri wa fedha za mapato na matumizi kwa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa, kuwasilisha andiko la Mradi linaonyesha manufaa ya kiuchumi na kijamii yatakayopatikana baada ya kuanzishwa, uwezo wa kurejesha mkopo kwa wakati na taarifa ya tathimini ya Mazingira (Environmental Impact Assessment)
…”ninafahamu dhahiri kwamba fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani katika Halmashauri nyingi hapa nchini ni Kidogo, kwa maana hiyo, Mikopo ni njia ya nyongeza ya kupata fedha ili kuzisaidia Halmashauri kutimiza malengo yake”
Akizungumzia Miradi iliyokwisha tekelezwa kwa fedha za mikopo toka Bodi hiyo, Mhasibu wa Bodi Mourice Kopalogira alisema kuwa mpaka sasa Bodi imeweza kutoa mikopo kwenye baadhi ya Mamlaka za Serikali Za mitaa na kuziwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ambapo miradi hiyo imekwa na manufaa makubwa kwa kuziongezea mamlaka husika mapato, fursa za ajira, shughuli za kiuchumi na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na huduma. Mpaka sasa miradi iliyopata mikopo ni pamoja na Ujenzi wa masoko,Vituo vya mabasi kumbi za mikutano, kilimo cha mazao ya tumbaku na zabibu.
Sanjali na Miradi hiyo, Miradi ya Uzalishaji Umeme, Upimaji viwanja, Ujenzi wa Majengo ya Utawala, ununuzi wa zana za ujenzi, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na miradi ya uvuvi imekopeshwa pia.
Kopalogira alisema kuwa licha ya kupata mafanikio lukuki, bado kuna changamoto ambazo Bodi imekuwa ikikumbana nazo ikiwemo uwasilishwaji wa michango na urejeshaji usioridhisha, Mtaji kuwa mdogo na baadhi ya serikali za Mitaa kukosa Mwamko wa Kimaendeleo.
….Mahitaji ya mikopo kuwa mikubwa kuliko uwezo wa Bodi. Kwa Mfano, Bodi hadi mwishoni mwa Novemba 2013, imeweza kutoa mikopo ya Shilingi 6.9 bilioni sawa na asilimia 16 tu ya Maombi yaliyopokelewa ya Tsh.43.1 bilioni. Ili tutelezeleza jukumu letu vema tunatafuta mtaji wa Bilioni 50 kuanzisha Benki yetu ya Maendeleo. Katika fedha hizo, Serikali kuu itatupatia Tsh.17 bilioni, Mamlaka za Serikali za Mitaa Tsh.11 bilioni na Wadau wa Maendeleo watatupatia Tsh.22 Bilioni. Fedha hizi zitatumika kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa. aliongeza kusema.
Benki hii itaendeshwa na Watumishi wa Serikali za Mitaa wenye utaalam wa Kibenki na itakuwa na madirisha mawili moja litashughulikia miradi ya Maendeleo na jingine mtu mmoja mmoja na itakuwa na riba nafuu. Hayo yalielezwa na Kopalogira baada ya kuulizwa swali na Marco Mangu aliyetaka kujua kama benki hiyo itatoa riba nafuu kwa watumishi.
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Addhu Dadi Mkomambo aliushukuru ugeni huo na kusema sasa imefika wakati kwa Halmashauri kutekeleza miradi yote ya maendeleo kwa kuwa sehemu ya kupopa tena kwa riba nafuu imepatikana. Huu ni ukombozi kwetu alisema.
Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ni Taasisi ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Bodi hii iliundwa chini ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 Sura Namba 290.