Mwenyekiti wa Taifa, Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), John Heche.(Picha na Maktaba)
Na Mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), John Heche, ametangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Septemba 10, mwaka huu kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Heche alisema anaheshimu Katiba ya chama hicho ambapo kutokana na umri wake kuvuka miaka 30, hatagombea tena nafasi hiyo.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu utasimamiwa na waangalizi wengine kutoka nchi mbalimbali wataalikwa kutokana na Bavicha kujenga mahusiano mazuri na vijana kutoka nchi nyingi za Ulaya.
“Kwa sasa nina umri wa miaka 32, kikatiba na mwongozo wa chama chetu, siwezi kugombea na mimi naheshimu hilo lakini tumefanya mambo mengi kwani chama ni vijana na sisi tumehakikisha kuanzia ngazi ya shina, matawi, kata,wilaya na jimbo tumeweka viongozi hivyo tupo imara kuanzia ngazi ya chini,” alisema.
Aliongeza kuwa, uchaguzi wa mwaka huu watausimamia kikamilifu kwa kuondoa vibaraka wote wanaoendeshwa kwa ‘rimoti’ na wale ambao itabainika wametoa rushwa ili kupata uongozi, watachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).
“Hatupo tayari kuona uchaguzi unafanyika katika mazingira ya rushwa na watu wasio na sifa kuongoza baraza hili kwani uchaguzi uliopita ulitawaliwa na vurugu kubwa,” alisema Bw. Heche.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa baraza hilo, Deogratias Munishi, alisema hadi sasa baraza hilo limeunda misingi zaidi ya 250 na matawi 19,000 nchi nzima.
Aliongeza kuwa, hadi kufikia Agosti 15, mwaka huu ngazi za majimbo na wilaya zinapaswa kukamilisha chaguzi zake na Agosti 30, mwaka huu ngazi zote za mikoa ziwe zimefanya chaguzi zake zote.
“Nami natangaza rasmi kuwa umri wangu hauniruhusu kugombea tena Ukatibu Mkuu hivyo sitagombea.
Munishi alisema kuwa kuanzia Agosti 10-25, mwaka huu ni muda wa kuchukua na kujaza fomu za kugombea nafasi za uongozi ndani ya baraza ngazi ya Taifa.
“Uchaguzi wa mwaka huu unawahusu vijana wote waliozaliwa Januari mwaka 1984 si chini ya hapo, nafasi zinazogombewa ngazi ya majimbo, Wilaya na Mkoani Mwenyekiti, Katibu, Mratibu Muhamasishaji na Mweka Hazina,” alisema Bw. Munishi.
Alisema ngazi ya Taifa ni Mwenyekiti Taifa, Makamu Mweyekiti Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu kutoka Zanzibar na Bara, Mratibu Mhamasishaji Taifa na Mweka Hazina.
Nafasi zingine ngazi ya Taifa ni wajumbe watano wa kuwakilisha vijana kwenye Baraza Kuu la Chama hicho wanne kutoka Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, wajumbe 20 wa kuwakilisha vijana katika Mkutano Mkuu wa chama hicho ambapo wajumbe 15 watatoka Tanzania Bara na watano kutoka Zanzibar.