Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salumu.
Na Mwandishi wetu
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salumu amewaasa watanzania kusherehekea sikukuu ya Idd El fitri kwa uadilifu na kuacha dhambi kwani hazimpendezi Mwenyezi Mungu.
Akizungumza Jumapili asubuhi, Julai 27, 2014, alisisitiza kuwa kwa sasa jamii inapaswa kujiandaa vema na sikukuu hiyo na ni wakati mzuri wa jamii ya watanzania kuendelea kutenda mema
“sio kwamba kwa sababu watu wamemaliza kipindi cha mfungo, ndio wanaenda kusherehekea Idd kwa kufanya matendo maovu kama vile uzinzi, ulevi na starehe zingine zisizompendeza Mwenyezi Mungu, nawaasa Waislamu wote kwa taoufiq ya Mwenyezi Mungu wajiepushe na hilo” alisema
Aliongeza kuwa jamii ya watanzania sasa inatakiwa kushirikiana bila kujali tofauti za dini zao kwani wote ni watoto wa Mungu.
Alhadi alisema kuwa anashangaa sasa jamii inazidi kushamiri katika maovu, vijana wa kike na wa kiume wanatembea pamoja bila kufunga ndoa, na kila mtu anajisifu kuwa kila mtu na demu wake, na wazazi wanaona suala hilo bila kukemea.
Huku hayo yakishamiri, sheik huyo alisema kuwa hata hivyo anashangaa watu ambao wapo tayari kusherehekea wao peke yao bila wenzao kwa kuzingatia uwezo.
Wapo wenye uwezo waliojaliwa, tunaomba wawaalike na wale wasiojiweza ili tufurahi pamoja, tena bila kuzingatia tofauti za dini yetu kwani si vizuri kuonekana unasherehekea halafu mwenzako anakuangalia, alisisitiza Alhad Salum.