Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambambe (kulia) na Katibu Mwenezi wa Chama hicho na Mbunge wa Kigoma kusini Mh. David Kafulila.(Picha na Maktaba).
Na Mwandishi wetu
Chama cha NCCR Mageuzi kimefanya mkutano mkubwa wa hadhara Kigoma Mjini, huku ajenda kubwa iliyotawala mkutano huo ikiwa ni suala la wizi wa pesa katika akaunti ya Escrow, pamoja na utendaji unaodaiwa mbovu wa Spika wa bunge la Jamhuri Anna Makinda.
Wakihutubia wananchi wa Kigoma, Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambambe, Katibu Mwenezi wa Chama hicho na Mbunge wa Kigoma kusini David Kafulila, Mbunge wa Muhambwe Felix Mkosamali, walikemea suala la viongozi wa serikali kujitengenezea mazingira yaliyohalalisha wizi wa pesa hizo katika akaunti ya Escrow
Katika mkutano huo uliofanyika uwanja wa Mwanga, katikati ya mji wa Kigoma Mkosamali alisema Bunge la Tanzania sasa kwa mujibu wa taarifa za Transparency international ni taasisi inayopokea rushwa pengine kuliko taasisi zingine.
Mkosamali alisema kuwa Spika ameshindwa kufanya kazi ya kuongoza Bunge, badala yake anajificha katika kivuli cha Takukuru na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, katika kutekeleza majukumu yake bungeni
Kwa upande wake, David Kafulila alisema kuwa sasa sio wakati wa kulala, akiwaomba wananchi wa Tanzania wamuunge mkono kwani suala la pesa hizo zaEescrow ni la watanzania wote kwani pesa iliyoibwa ni ya watanzania.
Katika Mkutano huo Kafulila alisema pesa hizo zilitoka kwenye akaunti hiyo kwa shinikizo la ofisi ya Werema na Muhongo, na zilitoka Novemba mwaka 2013.