Afisa Habari Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwani Wema (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni , jijini Dar es Salaam kuhusu maonesho ya 15 ya wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi ya Jumuhiya ya Afrika Mashariki; yajulikanayo kama Nguvu Kazi/Jua Kali yanayotarajiwa kufanyika Kigali Rwanda,Novemba 30 hadi Desemba 7 mwaka huu. Kulia ni Afisa Kazi Mwandamizi wa Wizara ya Kazi na Ajira, Sara Daudi.
Lorietha Laurence- Maelezo
Wajasiriamali wamehimizwa kujiandikisha kwa wingi ili waweze kushiriki katika maonesho ya 15 ya wajasiriamali ya sekta isiyo rasmi yanayoshirikisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yajulikanayo kama Nguvu ya kazi/Jua kali yanayotarajiwa kufanyika November 30 hadi desemba 7, 2014 mjini Kigali Rwanda.
Wito huo umetolewa na Afisa Habari Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwani Wema alipokuwa akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es salaam na kusema kwamba lengo la kuwahimiza wajasirimali kuweza kujitangaza nje ya nchi na kupanua wigo wa soko la bidhaa zao linadhamiria kuongeza ajira.
“nawaomba wajasiriamali waweze kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha na hivyo kuweza kushiriki maonesho haya ambayo yatajumuisha nchi za Afrika Mashariki na hivyo kuwapa fursa ya kupanua wigo wa soko kwa bidhaa zinaotengenezwa na wajasiriamali hao,” amesema Ridhiwani.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yana malengo ya kuongeza fursa za ajira kupitia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, kuchochea ubunifu, kupanua wigo wa masoko na kuwaunganisha wajasiriamali wadogo katika ngazi ya nchi na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Aidha alisisitiza kuwa ili mjasiriamali aweze kushiriki katika maonesho hayo ni lazima awe mzalishaji wa bidhaa inayohitajika katika maonesho, pia bidhaa hizo ziwe zenye ubora kwa kukubalika na ubora wa viwango (TBS) na viwango vya taasisi inayosimamia vyakula dawa,TFDA, kadhalika anuani ya kudumu ya mahali anapofanyia kazi mjasiriamali husika.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Tanzania, Joseph Rweyemamu aliongeza kuwa kuna umuhimu sana kwa wajasiriamali kushiriki maonesho haya kwa sababu ni njia mojawapo ya kujitangaza nje ya nchi kutokana na bidhaa zao.
Maonesho hayo yalianzishwa mwaka 1999 jijini Arusha, wakati wa kusainiwa kwa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na yamekuwa yakiendelea kufanyika kila mwaka kwa kuzunguka nchi zote za Afrika Mashariki, ambapo kwa Tanzania bara yalifanyika mwaka 1999,2006 na 2009.