Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii katika halmashauri ya wilaya ya Singida,Elia Digha,akitoa taarifa yake mbele ya kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
WAZAZI na walezi katika Halmashauri ya wilaya ya Singida mkoa wa Singida wameshauriwa kuchukua tahadhari didhi ya watu wanaojifanya ni madalali wa kuhamisha wanafunzi walioko shule za sekondari kwa madai kwamba kuna uwezekano mkubwa wakapoteza fedha na pia wanafunzi husika hawatakuwa na shule ya kujiendeleza kielimu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Elia Digha walati akitoa taarifa yake mbele ya kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi.
Amesema imebainika kwamba kuna watu wanaojifanya madalali ambao huwadanganya wazazi na walezi kwamba wanao uwezo mkubwa wa kuwatafutia watoto wao shule bora zaidi.
“Kwa mfano watamdanganya mzazi/mlezi kuwa wanao uhusiano mzuri na uongozi wa shule ya sekondari Kinampanda.Baada ya hapo,anaomba fedha ili aweze kumsaidia mtoto husika kumhamia kwenye shule hiyo”,alifafanua.
Digha amesema uchunguzi juu ya ulaghai huo,unaonyesha kwamba baadhi ya wanafunzi wanaohama shule za sekondati kupitia mbinu za udalali,hawapo kwenye shule walikohamishiwa.
“Hivyo tunawashauri wazazi watahadharishwe na hali hii,wazazi wawe wanataja mahali wanakohamia watoto wao na rekodi iwepo.Pamoja na ushauri huu,imeagizwa watoto waliohama/waliobadilisha shule,wafuatiliwe kama wapo kwenye hizo shule”,amesema Digha.
Wakati huo huo,Digha ambaye ni diwani wa kata ya Msange (CCM) jimbo la Singida kaskazini,amesema idara ya elimu ya sekondari katika halmashauri hiyo,inakabiliwa na chanagmoto nyingi,ikiwemo ya upungufu mkubwa wa walimu na watumishi wasio walimu.
Digha alitaja changamoto zingine kuwa ni pingufu wa miundombinu ya vyumba madarasa,nyumba za walimu,vyoo,madawati na serikali pia huwa inachelewesha kutuma fedha za uendeshaji.