Meneja wa Kampuni ya Vodacom mkoani Mbeya Emmanuel Sagenge (Kushoto) akikabidhi msaada kwa Mwenyekiti wa mtandao wa watoto mkoa wa Mbeya Zahara Mansoor, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika kituo cha kulea watoto yatima cha Nuru Orphans Centre kilichopo Uyole Jijini Mbeya. Msaada huo utagawanywa katika vituo vitatu ambavyo niNuru, Iwambi na Chipro vyote vipo jijini Mbeya.
Wafanyakazi wa Vodacom mkoani Mbeya mjini wakishusha vitu kwenye gari ikiwa ni moja ya msaada iliyotolewa na kampuni hiyo kwenye vituo vya kulea watoto yatima mkoani Mbeya vikiwemo Nuru Orphans Centre, Iwambi Orphans Centre na Chipro Orphans Centre vyote vipo jijini Mbeya. Msaada huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni tatu.
Wito umetolewa kwa jamii ya Watanzania kujitolea kuwalea watoto yatima ili kupunguza wimbi la watoto wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu ili kuweka jamii yenye usawa na kujenga nguvu kazi imara ya taifa siku za usoni.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Yatima Mkoani Mbeya ambaye pia ni Meneja Mradi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Nuru Orphanage Centre kilichopo uyole Mkoani Mbeya Bi. Zahara Mansoor wakati akipokea msaada wa unga wa sembe, sabuni, mafuta ya kupikia, mchele, maharage, maziwa na chumvi pamoja na pamoja vifaa vya shule kama vile; penseli, kalamu, madaftari, miswaki,kutoka kwa wafanyakazi wa Vodacom Tanzania wa Mkoani humo.
Mkurugenzi huyo amesema tatizo la watoto yatima limekuwa changamoto kubwa katika jamii hususani katika nchi zinazoendelea huku bado watoto hao wakikosa sehemu ya kuishi au mahali pazuri pa kulelewa kufuatia watu wengi wanaojitolea kuwalea watoto hao kukosa uwezo wa kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
“Ninapenda jamii itambue kuwa jukumu la kulea watoto yatima sio la watu fulani wachache tu ni jukumu letu sote kuhakikisha tunaunganisha nguvu kazi na kuwa na nyoyo za upendo katika kuwalea watoto hawa, ili tujenge jamii yenye usawa na nguvu mali ya taifa letu siku za usoni, wengi tunasema Watoto ni taifa la kesho yatima pia wanahitaji kupata nafasi katika taifa hilo la kesho hivyo ni lazima tujitolee kuwasaidia”, alisema Bi. Mansoor
Bi. Zahara aliongezea kuwa ni vema kwa makampuni na taasisi mbali mbali kujenga utamaduni wa kujitolea kwa ajili ya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na sio kuwaachia jukumu hilo wenye vituo pekee.
“Ninawashukuru wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kwa msaada wao, msaada huu utatusaidia katika vituo vyetu vitatu vya Chipro, Iwambi na Nuru,Pia napenda kutoa wito kwa Watanzania kujitolea katika kuwasaidia watoto hawa.
Kwa upande wake Meneja wa Vodacom Mbeya mjini, Emmanuel Sagenge alisema kampeni ya Pamoja na Vodacom ni matokeo ya kuguswa kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na matatizo mbali mbali yanayoikumba jamii inayowazunguka na kuamua kutoa sehemu ya kipato chao katika kuwasaidia yatima.
“Ni jambo la ujasiri kwa waanzilishi wa vituo vya kulea watoto yatima nchini kwani si kila mtu anaweza kufanya hilo, sisi kama wafanyakazi tunao wajibu wa kuwezesha vituo hivi kwa kile tunachokipata kutokana na kufanya kazi kwetu ili kuwatia nguvu na hata kuwahamasisha wengine wafanye hivyo.” Alisema Bw. Sagenge.
Meneja huyo alimalizia kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo hawataishia hapo kwani zoezi hilo ni endelevu itahakikisha popote pale huduma zao zilipo basi na wao watawafikia wote wanaohitaji msaada. Na kisha kutoa wito kwa taasisi na watu binafsi pamoja na wafanyakazi wa sekta ya simu kuiga mfano wao na kuwa na utamaduni wa kujitolea kusaidia ama kulimaliza kabisa swala zima la kuwasaidia watoto waishio katika mazingira magumu kwani bado safari ya kuwa na jamii bora ni ndefu.