Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilayani Ikungi, Olivary Kamilly akitoa taarifa yake wakati wa makabidhiano ya majukumu kati ya kamati iliyomaliza muda wake na ile inayotarajiwa kuanza kazi Januari mwakani.Kush oto ni diwani (CCM) kata ya Ikungi, Haji Mukhandi na katikati ni mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo aliyemaliza muda wake Naftal Gukwi.
Diwani wa kata ya Ikungi wilaya ya Ikungi,Haji Mukhandi akitoa nasaha zake wakati wa hafla ya makabidhiano baina ya kamati ya shule ya msingi Ikungi mchanganyiko iliyofanyika shuleni hapo.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Ikungi mchanganyiko aliyemaliza muda wake, Naftali Gukwi (kulia) akikabidhi hati ya makabidhiano Mwenyekiti mteule, mwalimu mstaafu,Rashid Msaru.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Ikungi mchanganyiko na baadhi ya walimu,wakifuatilia ajenda za mkutano wa dharura wa kamati ya shule hiyo.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Ikungi
MWALIMU Mkuu wa shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko Wilaya ya Ikungi, Olivery Kamilly amewataka wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni ili pamoja na mambo mengine kuthibiti utoro unaochangia kushusha kiwango cha taaluma.
Kamilly ametoa changamoto hiyo hivi karibuni wakati akizungumza muda mfupi baada ya kamati ya zamani kukabidhi majukumu kwa kamati teule inayotarajiwa kuanza kazi Januari mwakani.
Amesema utoro wowote uwe wa reja reja au ule sugu unachangia mwanafunzi asiwe na mtiririko mzuri wa masomo.
Akifafanua zaidi amesema,“Matunda ya utoro ni mwanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani yao. Ili hili lisitokee tena ushirikiano baina ya wazazi na walezi, walimu na kamati ya shule uimarishwe ili kudhibiti utoro kwa wanafunzi”.
Aidha, mwalimu Kamilly alitaja baadhi ya majukumu ya kamati ya shule kuwa ni pamoja na kusimamia uandikishaji wa elimu ya awali na wa darasa la kwanza.
Alitaja majukumu mengine kuwa ni kuhakikisha shule inajitosheleza kwa miundo mbinu bora kwa vile majengo, samani na vifaa vya kujifunzia na kujifundishia na kubuni na kutafuta vyanzo vya mapato kwa ajili ya kugharamia shughuli zilizopo kwenye mpango wa maendeleo ya shule.
Kwa mujibu wa mwalimu Kamilly, shule hiyo iliyoanzishwa 1944, inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya ukosefu wa ushirikiano wa baadhi ya wazazi na uongozi wa shule na hasa wazazi wenye watoto wenye ulemavu.
“Pia shule haina mtandao wa mabomba ya maji shuleni na hii inasababisha watoto wenye ulemavu wa uoni na ngazi kufuata maji kwa matumizi yao umbali mrefu ambao ni hatari kwa maisha yao”,amesema mwalimu Kamily.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mteule wa kamati ya shule hiyo, Rashid Msaru aliahidi kuwa kamati yake itakuwa daraja zuri kati ya shule na serikali za vijiji, na kati ya walimu na wazazi na walezi.
Aidha, Msaru aliahidi kuwa kamati yake itakuwa ni ya maendeleo ya shule tu na wala siyo ya kudhibiti walimu.