Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua shamba la Minazi la Serikali la ekari 45 lililo chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi likikabidhiwa kwa Wizara ya Kilimo kwa vile lipo katika Ukanda wa Utafiti wa Kilimo katika Kijiji cha Tumbe Mkoa Kaskazini Pemba.
Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asil zisizorejesheka Pemba Nd. Said Juma Ali akielezea hatua zilizochukuliwa na Wizara ya kilimo katika kuotesha minazi kwenye eka 10 zilizomo ndani ya shamba la Serikali la ekari 45 liliopo katika Kijiji cha Tumbe Kaskazini Pemba.
Sheha wa Shehia ya Micheweni Mjini Bw. Dawa Juma Mshindo akielezea changamoto wanazopambana nazo Masheha Kisiwani Pemba mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliokutana nao katika Ukumbi wa Chuo cha Amali Kilichopo Vitongoji vya Chake Chake Pemba. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa uamuzi kwamba Mashamba yote ya Mikarafuu na Minazi ya Serikali yaliyokuwa chini ya Usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia sasa yatakuwa yakishughulikiwa na Wziara ya Kilimo na Mali Asili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa uamuzi huo wa Serikali wakati akizungumza na Masheha wote wa Mikoa Miwili ya Pemba katika ukumbi wa Chuo cha Amali Vitongoji vya Chake Chake Pemba.
Balozi Seif amesema wakati suala la Ardhi litaendelea kubakia Wizara ya Ardhi, amewaomba Masheha ambao maeneo yao yamo Mashamba ya Serikali ya Mikarafuu na Minazi na hadi sasa hayajahakikiwa watoe Taarifa kwa Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Pemba au Kiongozi yeyote atakayewekwa kwenye zoni.
Ameema udhibiti wa mapato yanayotokana na mazao yaliyomo kwenye baadhi ya mashamba ya Serikali yalikuwa yakileta mgongano kutokana na Mashamba hayo kushughulikiwa na Wizara mbili tofauti.
Wakielezea changamoto zinazowakabili baadhi ya Masheha hao wamesema mazingira duni wakati wanapostaafu utumishi wao pamoja na mfumko wa hujuma wanazofanyiwa masheha limekuwa tatizo kubwa linalopunguza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.
Masheha hao wameiomba Serikali Kuu kujenga mazingira yatakayowawezesha kupatiwa mikopo ya vyombo vya usafiri ili kurahisisha kazi zao, masuala ambayo Balozi Seif ameahidi kwamba Serikali itayazingatia na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.
Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asili zisizorejesheka Pemba Nd. Said Juma Ali alimueleza Balozi Seif kwamba Ekari kumi tayari zimeshaoteshwa minazi mipya ya asili (East Africa).
Nd. Ali amesema kituo cha Utafiti wa Kilimo Pemba kinaendelea na harakati za kurejesha minazi ya asili kwa kuotesha mbegu zitakazouzwa kwa wakulima katika maeneo mbali mbali ili kuziba pengo la minazi mipya ambayo uzalishaji wake huchukuwa kipindi kifupi.