Katika kuimarisha utendaji wa shule, Wakuu wa shule za sekondari 3,001 wamepatiwa mafunzo ya kuimarisha utendaji wa kazi zao kwa lengo la kuleta Matokeo Makubwa Sasa (MMS) kwenye sekta ya elimu. Mafunzo haya yalilenga kuwawezesha wakuu wa shule kusimamia na kuendesha shule kwa ufanisi.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa anasema kuwa atahakikisha kiwango cha elimu kinapanda ikiwemo ufaulu katika ngazi zote za elimu nchini kwa kuanzia na maboresho yanayaofanyika kupitia utekelezaji mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta ya elimu.
Mafunzo haya yalitolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) katika vituo vya Njombe, Magu, Bagamoyo na Arusha kati ya tarehe 23/09/2013 hadi tarehe 09/10/2013.
Wakuu wa shule za sekondari wakiwa mafunzoni katika kituo cha Magu.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (MMS) katika Sekta ya Elimu umeanza kutekelezwa mwezi Julai 2013 na unalenga kuboresha ubora wa Elimu katika ngazi ya Msingi na Sekondari. Utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa unahusisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inayohusika na Sera, ufuatiliaji na tathmini na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI) kupitia Halmashauri ambazo zinahusika katika usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi na sekondari. Wizara imeunda kitengo cha ufuatiliaji (Ministerial Delivery Unit – MDU) chenye jukumu la kumsaidia Waziri na Katibu Mkuu kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mradi na kutoa taarifa kwa viongozi hao.
Kupitia utaratibu Maabara, sekta ya elimu iliibua mikakati tisa kwa ajili ya kuleta Matokeo Makubwa Sasa (MMS). Mikakati hiyo ni; Kiongozi cha Usimamizi wa shule, Programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzajia, Upangaji wa shule kwa ufaulu kwa kuzingatia matokeo, upimaji wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na mafunzo kwa walimu kuhusu ufundishaji wa KKK, Utaratibu wa kutoa tuzo kwa shule, ruzuku ya uendeshaji shule, ujenzi wa miundombinu ya shule na motisha kwa walimu.
Pamoja na kutoa mafunzo kwa wakuu wa shule ya namna ya kutumia Kiongozi cha Usimamizi wa shule, Mikakati mingine ya MMS iliyoanza kutekelezwa ni program ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji. Wanafunzi 163,763 wa kidato cha nne mwaka 2013 walifanya mitihani wa majaribio kwa masomo ya Hisabati, English, Kiswahili na Biologia ili kupima uwezo wao. Aidha, walimu 4,064 wamepatiwa mafunzo yenye lengo la kuwasaidia wanafunzi kwenye maeneo yenye changamoto ya ujifunzaji.
Kwa upande wa elimu ya msingi, upimaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la pili ulifanyika kati ya tarehe 21 Oktoba na tarehe 4 Novemba 2013. Upimaji huo ulifanyika kwa kutumia zana maalum iliyoandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mwalimu akifanya tathmini ya kupima uelewa wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu katika shule ya msingi Mbutu, Manispaa ya Temeke.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa anasema:
“Katika kipindi cha miezi minne tangu kuzinduliwa kwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Sekta ya Elimu, tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii ili kuinua ubora wa elimu kwa watoto wete na, kwa kufaanya hivyo tutajenga mhimili wa kuendeleza Taifa letu.“
“Tumedhamiria kuinua viwango vya ubora na ufaulu wa wanafunzi katika elimu ya msingi na sekondari. Dhamira hii itafikiwa kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake bila kufanya makosa. Wizara yangu itahakikisha ubora wa elimu unaongezeka katika ngazi zote.“
Wizara pia imekamilisha zoezi la upangaji wa shule “School Ranking“ ya matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa mwaka 2012 na mwaka 2013 na vile vile Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 na kuweka kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (www.necta.go.tz) na tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (www.moe.go.tz)
Upangaji huu umeziweka shule kwa ubora wa matokeo ya kitaifa ambao utaongeza uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika usimamizi wa utoaji wa elimu bora. Shule zimepangwa kwa rangi nyekundu, njano na kijani kulingana na kiwango cha ufaulu. Shule zenye ufaulu wa chini zimepangwa katika kundi la rangi nyekundu, ufaulu wa kati zimepewa rangi ya njano na rangi ya kijani ni zenye ufaulu wa juu. Upangaji huu unalenga kuzisaidia zaidi shule zilizo na ufaulu mdogo.
Utekelezaji wa baadhi ya Mikakati ya MMS katika Sekta ya Elimu umeanza na upo katika hatua mbalimbali kama inavyoonyeshwa katika taarifa hii, ni matumaini yetu kuwa wadau wote wa elimu na jamii kwa ujumla wataendelea kuunga mkono mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika kuboresha elimu nchini.
Kutekelezwa kwa ufanisi mikakati mbalimbali ya elimu kutachangia kuinua ubora wa elimu itolewayo kwa wahitimu katika ngazi zote na hatimaye kuongeza nguvu kazi ya Taifa na kuinua uzalishaji.