Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Madaktari wako wapi?

$
0
0

surgery

Jumla ya Madaktari 890 kati ya 2,246 (ambayo ni sawa na 39.6%) ya Madaktari wenye shahada nchini Tanzania hawafanyi kazi ya kitabibu badala yake wanafanya kazi zingine. Aidha imebainika kuwa madaktari 964 (sawa na asilimia 42.9) tu wahitimu wa shahada ya udaktari ambao hufanya kazi katika hospitali na vituo ya kutolea huduma. Madaktari waliobakia ama wako masomoni, wanafanyakazi katika asasi za kiraia (AZAKI). wako katika taasisi mbalimbali za afya zinazojishughulisha na tafiti, mafunzo ama kufanya kazi katika Wizara ya Afya na wengine hufanya kazi katika taasisi zisizojishughulisha na masuala ya afya kabisa.

Haya yamebainika kwenye utafiti uliofanywa na shirika la Sikika kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kati ya mwezi Agosti na Oktoba, 2012 ambapo jumla ya madaktari 2246 walishiriki.

Utafiti huo umeonyesha pia kuwa karibia nusu ya Madaktari wote walioshiriki utafiti huo, wanaishi na kufanyakazi Arusha, Mbeya, Dar es Salaam na Moshi. Dar es Salaam pekee ikiwa na jumla ya madaktari 725 kati ya 2,246.

Utafiti huu umeonyesha kuwa karibia nusu (madaktari 48 kati ya 107) ya wahitimu wa mwaka 2003 hawafanyi kazi ya utabibu, wakati huo huo madaktari 68 kati ya 102 (sawa na theluthi mbili) ya wahitimu wa mwaka 2004, zaidi ya robo tatu (176 kati ya 224) ya wahitimu wa mwaka 2008 na 155 kati ya 206 ya wahitimu wa mwaka 2009 wanafanya kazi za kitabibu.

Jumla ya madaktari 246 kati 290 (sawa na asilimia 85) ya wahitimu wa mwaka 2011 walikuwa hawafanyi kazi ya utabibu wakati utafiti huu ukifanyika. Karibia madaktari wote (96 kati ya 101) waliohitimu masomo yao mwaka 2012 wanafanya kazi ya utabibu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa Tanzania ina uwiano wa Daktari mmoja kwa kila watu 30,000 (kwa maana nyingine; daktari mmoja nchini Tanzania huhudumia takribani watu 30,000). Uwiano huu haujaboreka sana katika miaka ya hivi karibuni kutoka na ungezeko la idadi ya watu hapa nchini.

Mapendekezo

Kutokana na matokeo ya utafiti huu, Sikika na MAT wanapendekeza kuwepo kwa juhudi za makusudi za Serikali na wadau za kuwavutia madaktari kufanya kazi za kutoa huduma za kitabibu katika vituo vya kutolea huduma. Juhudi hizo ziende sambamba na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kuwabakiza hapa nchini badala ya kukimbilia nchi nyingine.

Kuna haja ya uwepo wa mfumo, sheria na taratibu mpya zitakazowezesha madaktari walioko katika sekta zingine waweze kutumia muda fulani kufanya kazi ya utabibu ili kuwapunguzia mzigo wa kazi madaktari wanaotoa huduma za kitabibu mahospitalini.

Aidha, kwa kuwa madaktari wengi pamoja na huduma nzuri za afya hupatikana maeneo ya miji mikubwa, kuna haja ya kuboresha miundombinu na kuimarishwa kwa mfumo wa rufaa ili kuwawezesha wananchi wote, bila kujali maeneo wanayoishi, waweze kupata huduma za afya zenye viwango vya juu.

Hata hivyo, inapaswa kufanyika kwa tafiti nyingi zaidi ili kubaini sababu zinazopelekea wimbi kubwa la madaktari kuacha kufanya kazi ya utabibu mahospitalini ili kuweza kupunguza upotevu wa rasilimali watu.

Kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi na kamili, mifumo ya taarifa iliyopo iboreshwe ili iweze kukusanya na kutunza taarifa na kumbukumbu za mahali walipo madaktari na wataalamu wengine wa afya na kama wanatoa huduma au laa!. 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles