Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea na kuisoma Ripoti Kuhusu Ushindani wa Kibiashara Duniani (Global Competitiveness Index – GCI) itolewayo kila mwaka na Asasi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum (WEF) baada ya utafiti wa kina katika nchi karibu zote duniani.
Kufuatia Ripoti hiyo na matokeo ya utafiti huo wa WEF, Rais Kikwete amewasiliana na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (National Investment Steering Committee) na kutoa maelekezo yafuatayo:
Kwamba, Mheshimiwa Pinda na Kamati yake wakae chini, waisome Ripoti hiyo, waichambue na kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusu hatua gani zinastahili kuchukuliwa kuhusu Ripoti hiyo kwa nia ya kuongeza ushindani wa kibiashara nchini na kuboresha nafasi ya Tanzania katika Ripoti hiyo mwaka ujao.
Kwamba, Waziri Mkuu na Kamati yake wamfikishie Mhe. Rais ushauri wao katika muda wa mwezi mmoja tokea jana Jumatatu, Septemba 9, 2013.