Mwandishi wa Habari Daniel Makaka wa redio Sengerema mkoani Mwanza akizungumza na Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Kilanga Maganya kuhusiana na tatizo la Uhaba wa Maji wilaya ya Sengerema.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema Bw. Nelson Rwelengela akiongea na Mtandao wa Habari wa Mo Blog kuhusu tatizo la uhaba wa Maji katika shule yake.
Na. Mo Blog, Sengerema.
Uhaba wa Maji katika mji wa Sengerema mkoani Mwanza umeathiri masomo katika shule ya Sekondari Sengerema iliyopo Wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema Bw. Nelson Rwelengela alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa tatizo la Maji linaloukabili mji wa Sengerema limesababisha Wanafunzi wa Shule hiyo kuchukua muda mrefu kutafuta maji na kusababisha kukosa vipindi vingi vya masomo.
Aidha amesema kuwa pamoja na Wanafunzi hao kufuata maji hayo umbali mrefu katika Bwawa la Mzungu , maji hayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Wanafunzi wa shule ya Sekondaro Sengerema, wamekuwa wakikumbwa na magonjwa mbali mbali ikiwemo Homa ya Matumbo (Typhoid) na Minyoo ya Tumbo, yanayosadikiwa kusababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
Akithibitisha tatizo hilo, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Bw. Kilanga Maganya amekiri tatizo la Maji ni changamoto kubwa katika Wilaya nzima ya Sengerema na kwamba limedumu kwa muda mrufu sasa bila kupatiwa ufumbuzi.
Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilijaribu kutatua tatizo la Maji katika shule hiyo kwa kuchimbia Visima, zoezi ambalo halikuwafanikiwa kutokana na kukosa Maji sehemu hiyo
Bw. Maganya amesema, pia wanatarajia kuanza kutumia utaratibu wa kuanza kuvuna maji ya mvua, hivyo Idara yake inawasiliana na Wizara kuona uwezekano wa kupata matanki yatakayotumika kuhifadhia Maji ya Mvua yatakayovunwa.
Katika jitihada nyingine amesema Halmashauri ya Sengerema iko mbioni kumaliza tatizo hilo, kutokana na ufadhili mkubwa wa Benki ya Africa unaofadhili mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria hadi Wilayani Sengerema.
Hivyo ameiomba Serikali kuharakisha jitihada hizo ili kuondoa tatizo la maji wilayani Sengerema.
Mwandishi wa habari wa redio Sengerema na mwakilishi wa mtandao wa habari wa Mo Blog Daniel Makaka akifanya mahojiano na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema Bw. Nelson Rwelengela.
Bwawa la Mzungu lililopo Wilaya ya Sengerema kata ya Ibisabageni mkoani Mwanza linalotumika kwa matumizi ya Maji ya kupikia na kunywa kutokana na Uhaba wa Maji katika Mji wa Sengerema.
Mmoja wa wakazi wa Sengerema akivua Samaki ndani ya Bwawa hilo.
Baadhi ya Wakazi wa Wilaya ya Sengerema wakioga ndani ya bwawa hilo kutokana na uhaba wa Maji uliogubika mji wa Sengerema.
Picha juu na chini ni Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sengerema wakitoka kuchota Maji umbali mrefu kutokana na uhaba wa Maji shuleni hapo ambapo suala hilo linachangia kupoteza muda wa masomo na kuililia Serikali iwaangalie kwa jicho la pili.
Baadhi ya watoto wakifua nguo zao kando kando ya Bwawa hilo lenye Maji yasiyo Safi na Salama kwa matumizi ya Binadamu.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Sengerema wakiteka Maji ya matumizi ya kupikia na kunywa katika Bwawa hilo.
Mwandishi wa Redio Sengerema na Mwakilishi wa Mtandao wa Habari wa Mo Blog Makaka Daniel akifanya mahojiano na mkazi wa Mjini Sengerema Bi. Miyango Slyvester kama alivyokutwa na Camera ya Mo Blog akifua kando kando ya Bwawa hilo.
Baadhi ya Mifugo ikinywa Maji ndani Bwawa hilo kama ilivyokutwa na Camera yetu.
Baadhi ya wakinamama wakirejea makwao na ndoo za Maji waliyochota katika Bwawa la Mzungu lililopo mjini Sengerema.