Rais Vladimir Putin wa Russia amepiga marufuku maandamano wakati wa michezo ya Olimpiki ya msimu wa majira ya baridi kwa mwaka ujao wa 2014.
Katika kufanikisha utekelezaji wa amri hiyo, watu mbalimbali kuanzia katika viwanja vya michezo, bandari, vituo vya treni na vituo vya ukaguzi wa barabarani ambavyo vitakuwa maeneo muhimu ya ukaguzi watakaguliwa pamoja na mizigo yao.
Amri hiyo ya rais ambayo imechapishwa katika gazeti la serikali Rossiyskaya Gazeta, imeweka maeneo maalumu ya usalama katika jimbo la Sochi wakati wa michezo hiyo mwezi wa Februari katika eneo la mapumziko la bahari Nyeusi.
Amri hiyo pia imeweka “ukanda wa marufuku” kwa kuzuia kuingia katika maeneo ya michezo ya Olimpiki pamoja na sehemu kubwa ya mji wa Sochi.
Aidha amri hiyo imepiga marufuku kuvuka mpaka na kuingia katika eneo la waasi la Abkhazia nchini Georgia, ambalo lipo umbali wa kilometa kadhaa kutoka katika uwanja wa michezo ya Olimpiki.
Mpango wa Putin umezuia maandamano yoyote ambayo hayahusiani na michezo ya Olimpiki katika eneo husika kuanzia Januari 7 mpaka Machi 21, 2014.-DW.