Na Nathaniel Limu, Ikungi
BAADHI ya Viongozi wa vyama siasa vya upinzani walioshinda nafasi za Serikali za vijiji, vitongoji na mitaa wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida kwenye uchaguzi uliopita, hawajui majukumu yao na wanadhani kuwa wamechaguliwa kupinga viongozi wa CCM tu; imeelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Aluu Segamba, alisema kwamba viongozi hao hawatambui kwamba baada ya kushinda nafasi hizo, wanapaswa kuwatambua na akuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi wa aina yo yote, ikiwemo itikadi za kisiasa.
Akifafanua, alisema toka viongozi hao na hasa wale wa CHADEMA wanyakue nafasi hizo, kazi yao kuu imekuwa ni kupinga kila kitu ambacho viongozi wa CCM wanakifanya au kushauri na pia wameelekeza nguvu zao kujaribu kupora nyumba zinazomilikiwa kihalali na CCM.
“Viongozi hawa kwa sababu ni wageni katika nafasi hizo za uongozi, ni lazima watambue kuwa wao kwa sasa ni viongozi wa wananchi wa vyama vyote vya siasa na wasio na vyama katika eneo husika. Kwa hiyo ni lazima awashirikishekikamilifu katika masuala yote ya maendeleo.”,alisema Aluu na kuongeza kwa kusema kuwa;
“Akianza kupinga kila kitu cha maendeleo kinachopendekezwa na chama cho chote ambacho si chake, tabia hiyo itadumiza maendeleo ya Wilaya Ikungi”.
Aidha,Aluu alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa mafunzo juu ya majukumu na mimpaka ya viongozi wa serikali za vijiji, mtaa na vitongoji na kudai kuwa kwa njia hiyo itasaidia kuwajengea uwezo zaidi viongozi hawa kuwatumikia wananchi.
Katika hatua nyingine,Katibu huyo amewakumbusha wakuu wa idara katika halmashauri ya wilaya Ikungi kujenga utamaduni wa kutembelea mara kwa mara vijijini kuwahudumia wananchi, ili kuharakisha upatikanaji wa ufumbuzi wa kudumu dhidi kero zinazowakabili.
Wakati huo huo, Aluu amewasihi viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali wahimize waumini wao kusoma kwa kina Katiba iliyo pendekezwa, na wawape uhuru bila mashinikizo ya aina yo yote kuipigia kura ya maoni Katiba hiyo.