Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam
Wakurugenzi Wakuu wa Ofisi za Takwimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda, Uganda, Kenya, Burundi na Tanzania wamekutana leo jijini Dar es salaam kujadili mchango wa matumizi ya Takwimu sahihi katika kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Akifungua Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoka Tanzania Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa mkutano huo pamoja na mambo mengine unazileta pamoja Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya Takwimu na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya nchi hizo.
Amesema kuwa mkutano huo umelenga kuongeza na kuimarisha ushirikiano baina ya Nchi Wananchama wa Jumuiya hiyo katika matumizi ya Takwimu pamoja na kupitia mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazosimamia masuala ya Takwimu kwa Nchi Wanachama.
Kwa upande wao wakurugenzi hao kutoka Rwanda, Uganda, Kenya, na Burundi wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania kunatoa matumaini ya mwendelezo wa ushirikiano katika matumizi ya takwimu sahihi kutokana na mchango wake katika maendeleo ya nchi zao na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Wamesema kuwa nchi zao zitaendelea kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi mzuri wa takwimu mbalimbali zikiwemo za kilimo, Viwanda, Biashara, uchumi na takwimu nyingine kwa manufaa ya wananchi wa Jumuiya hiyo.
Kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania ambao umehusisha wakurugenzi wakuu, wakurugenzi na maafisa wandamizi wa takwimu ni mwendelezo wa mikutano mbalimbali inayofanyika katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kujadili mchango wa matumizi ya Takwimu sahihi katika kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.