Na Abdulla Ali-maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kuwapatia nyenzo za kufanyia kazi Askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ili liweze kujiendesha na kujiinua kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,. Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheri (pichani) wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor Juma katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema vijana wengi wanaoajiriwa kupitia Jeshi hilo ni kwa ajili ya kuwapa mafunzo ya kizalendo na kujifunza mbinu za utendaji kazi ikiwemo Ufundi, Kilimo, na Ujasiriamali na katika kufanikisha hilo Serikali imekuwa ikiwapatia nyenzo za kufanyia kazi kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu.
Amefahamisha kuwa kwa sasa Serikali imeshawapatia vifaa vya kilimo ikiwemo Matrekta, vifaa vya Ufundi, vifaa vya shughuli za Mifugo na kwa sasa Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya uvuvi kwa Jeshi hilo na kuiomba serikali kuwaongezea posho vijana wanaojiunga na Jeshi la JKU kwa kujitolea ili waweze kukidhi mahitaji yao.
Ametanabahisha kuwa Baraza la Wawakilishi limeshapitisha Sheria ya Wakala wa Ulinzi hatua ambayo itapelekea kuimarika kwa Jeshi hilo kiuchumi kama ilivyo kwa wenzao wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo wameweza kumiliki Shirika la Biashara la SUMA JKT pamoja na kampuni za ujenzi wa nyumba vinavyowasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Wakati huohuo akijibu swali la pili la mwakilishi wa jimbo la wawi amesema Wizara yake inaangalia uwezekano wa kupata fedha kutoka Wizara ya Fedha ya Zanzibar kwa ajili ya ununuzi wa matrekta na vifaa vyengine vya kilimo ambapo hadi sasa matrekta 2 aina ya FORD yameshapatikana ambayo yamegaiwa katika Kambi ya Kinumoshi Unguja na Kangagani kwa Pemba.
Vilevile amesema kwa upande wa miundombinu ya umwagiliaji maji Wizara yake imeshafanya mawasiliano na Wizara ya Kilimo na Maliasili na kukubaliana kupatiwa mashamba ya mpunga yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na mashamba hayo kuingizwa katika mradi mkubwa wa umwagiliaji Kitaifa ambao unafadhiliwa na Korea na Nchi nyengine wahisani.