Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Wajawazito Zanzibar washahuriwa kutumia vyakula vyenye lishe bora

$
0
0

02 (2)

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo.

Na Abdulla Ali na Mwanaisha Moh’d Maelezo-Zanzibar       

Kina mama wajawazito wameshauriwa kutumia vyakula vyenye Lishe Bora ili kuepukana na matatizo yanayoweza kujitokeza wakati wa kujifungua kwao.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.  Mahmoud Thabit  Kombo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor Juma katika ukumbi wa  Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.

Amesema ukosefu wa Lishe Bora kwa akina mama wajawazito ndio tatizo linalopelekea kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya kiafya ikiwemo akina mama hao kushindwa kujifungua katika hali ya kawaida jambo ambalo huhatarisha maisha yao.

Amefahamisha kuwa tatizo hilo husababishwa na ulaji wa vyakula visivyo vya asili ambavyo huwa na  kemikali ndani yake na kusababisha kukosekana kwa Homoni ya Chembe Chembe (Oxytocin) ambazo humrahisishia mama mjamzito kujifungua salama.

Ametanabahisha kuwa kutokana na ukosekanaji wa Chembe Chembe hizo Madktari hulazimika kumpatia mzazi kupitia njia mbadala zikiwemo za kumdunga sindano ili kuanzisha uchungu wakati inapotokea haja ya kufanya hivyo au kuufanya uchungu wenyewe uwe mkali zaidi kwa lengo la kuokoa maisha  ya mama mtoto.

Sambamba na hayo Mhe. Thabit Kombo amesema kutokuhudhuria katika vituo vya afya kwa wakati kwa kina mama wajawazito kwa ajili ya kupima na kupata ushauri wa kitaalamu  ni miongoni mwa matatizo yanayozorotesha afya ya mama na mtoto.

“Miongoni mwa matatizo yanayozorotesha afya ya mama na mtoto katika nchi yetu ni kushindwa kwa kina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati kwa ajili ya kupima ujauzito na kupata ushauri wa kiafya, lishe duni na kutojifungulia katika vituo vya afya”, Ameeleza Naibu huyo.

Amefahamisha kuwa wataalamu wa afya wanaweza kuyagundua matatizo hayo kwa urahisi kwa mama mjamzito ikiwa atahudhuria kiliniki kwani ndio njia mbadala ya kutambua matatizo ambayo yanaweza kijitokeza wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.

Naibu huyo amewashauri kina baba wawe wanawahudumikia kina mama wakati wa ujauzito kwa kuwapa vyakula vyenye lishe bora na kuhakikisha wanawasisitiza kuhudhuria kliniki ipasavyo ili kuweza kulinda afya na maisha ya mama na mtoto.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles