Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Unyanyapaa, Ukatili na Mauaji dhidi ya Albinism..Imetosha!

$
0
0

IMG_0904

Balozi wa kujitolea wa kampeni ya mapambano dhidi ya mauaji ya albino, Henry Mdimu (katikati) akizungumza na vyombo vya habari (hawapo pichani) wengine ni wajumbe wa kamati hiyo. Kushoto ni Monica Joseph na Kulia ni Masoud Kipanya.

IMG_0966

Baadhi ya wa Wajumbe wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mkutano wao  na waandishi wa habari.

..Sote kwa pamoja tuungane kupinga vitendo hivi viovu

Na Andrew Chale wa Modewji blog

“Sote kwa pamoja tuungane kupinga vitendo viovu wanavyofanyiwa  ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wenye Albinism. Tuseme imetosha! Unyanyapaa, ukatili na mauaji dhidi yetu”.

Hayo ni maneno ya Balozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi  na mwanahabari shupavu kutoka kampuni ya Mwananchi Communication, Henry Mdimu ambaye amejitolea kuwa balozi wa hiyari kupinga mauaji ya kikatili ya watu wenye albinism yanaoendelea nchini hususani mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwingineko.

Kauli hiyo, ameitoa jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari ambapo Mdimu ambaye ameungwa mkono na baadhi ya marafiki na watu wanaokerwa na vitendo hivyo, ikiwemo Chama cha Bloggers nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN), Masoud Kipanya  (Mchora vibonzo) na wengine wengi amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kushuhudia ndugu zake wakiteseka kwa muda mrefu dhidi ya mauaji hayo.

Balozi Mdimu amesema lengo lake kuu ni kuhakikisha anazunguka pamoja na marafiki watakao muunga mkono na kutoa elimu kwa kuanzia Kanda ya Ziwa ili tatizo hilo lisiendelee kuenea nchi nzima.

 Akifafanua zaidi alisema mauaji ya watu wenye albino yanaichafua Tanzania hivyo atahakikisha anaisaidia Serikali kupambana na watu wenye imani hizo za kipuuzi ili kuondoa doa linaloichafua nchi yetu ambayo imekuwa na sifa ya amani dunia nzima.

 “…Nimeamua kufanya hivi baada ya kushuhudia ndugu zangu wakiteseka kwa muda mrefu. Awali nilishindwa kuanzisha harakati hizi nikiamini kuna vyombo vinavyohusika na utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi.”

“…Hivyo nimeamua niweke jitihada zangu binafsi niisaidie Serikali yangu katika kuondoa doa hili linaloichafua Nchi yetu yenye sifa ya Amani duninia

nzima. Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu mniunge mkono tukishirikiana na Serikali ili mauaji haya yakome,” alisema Mdimu.

 “Kutokana na ushawishi nilionao kama Mwandishi, Mtangazaji wa redio na Blogger naamini nitaleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha haki ya kusihi kwa ndugu zangu inaheshimiwa na kubaki historia.

“Salamu zangu ziwafikie wanyanyasaji, wauaji na wenye kufanya dhihaka kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kuwa IMETOSHA.”

 Akifafanua zaidi alisema kwa uchunguzi wake wa awali umebaini ukosefu wa elimu juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi ndio chanzo cha tatizo hilo kukua na hatimaye kuuana kwa imani za kishirikina.

“…Hivyo basi, silaha ya Elimu ni sehemu kubwa ya haraki hizi,” alisisitiza Balozi huyo wa kujitolea.

Aidha alisema kuendesha harakati hizo alizozipa jina la ‘IMETOSHA’ elimu itatolewa kwa njia ya sanaa, na washauri nasaha pamoja na kundi la wanamuziki ambao pia wataandaa nyimbo mbalimbali za kutoa mafunzo ya kutokomeza ukatili huu.

Alisema wasanii ambao hadi sasa wamejitokeza kuunga mkono kampeni hizo ni paoma na Jhikoman, Kassim Mganga, Profesa J, Ray C, Fid Q, Roma Mkatoliki na Dami Msimamo.

Hata hivyo alisema bado pia anaamini nguvu ya vyombo vya habari ikiungana na kampeni hizo wanaweza kufanikiwa zaidi hivyo kuomba ushirikiano katika kuhakikisha vinapaza sauti kutokomeza mauaji hayo ya kikatili.

Msimamo wa Mo dewji blog:

Kwa upande wetu, mtandao huu unaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete dhidi ya mapambano kwa watu wanaofanya vitendo viovu kwa ndugu zetu kwa kuitaka jamii kuachana kabisa kwani imani potofu zimepitwa na wakati, zaidi tuwalinde, tuwapende na kushirikiana nao ndugu zetu wenye Albinism.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles