Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

EXCLUSIVE INTERVIEW: ‘Ushirikina chanzo cha mauaji ya watu wenye Albinism’– Dk. Ally Possi

$
0
0

Na Andrew Chale wa modewji blog

Dk. Ally Possi ambaye ni Mhadhiri wa chuo kikuu cha  Ardhi, Dar es Salaam. Akielezea na kuchambua kwa kina kuhusiana na wimbi la mateso na mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi wenye albinism.

Mo dewjiblog, iliamua kufanya mahojiano maalum ilikukuletea wewe msomaji wetu unayeperuzi mtandao wako bora kabisa kujua na kuelewa na nini kifanyike ikiwemo mimi na wewe katika kuchukua hatua.

Suala la mauaji dhidi ya watu wenye albinism:

“JAMII  yenye ushirikina ndio yenye kuamini suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa  ngozi ambao wana albinism, hivyo ilikuondoa imani hii potofu ni kutoa elimu katika maeneo yote na kuwalinda popote pale, Jambo hili ni jukumu letu sote”   anabainisha  Dk. Ally Possi.

Dkt. Possi anabainisha kuwa, Serikali itaendelea kulaumiwa mpaka hapo juhudi za dhati za kukomesha mauaji na vitendo vya kikatili vitakavyochukuliwa na kutokomezwa kabisa.

Fuatilia hapa Mahojiano hayo maalum.

DSC_0391

Mwanasheria na mhadhiri wa chuo kikuu cha Ardhi, Dk. Ally Possi akiwa kwenye ofisi za modewjiblog kabla ya mahojiano na mtandao huu. 

MO DEWJI BLOG : Karibu, mgeni wetu katika mtandao huu wa kijamii unaokuletea habari bora kabisa zilizochambuliwa  kwa kina za ndani, nje na makala maalum za kina.

DK. POSSI: Asante, nashukuru sana…

MO DEWJI BLOG: Unadhani nini chanzo na hali ya ongezeko la vitendo hivi kwa sasa hapa Tanzania?

DK.POSSI: “Kwanza mauaji ni.. yanatokana na imani potofu. Imani potofu kwa jamii kuwa ukipata kiungo cha alibino unafanikiwa.

Hii ni imani potofu kwa jamii ya watu wenye kuamini ushirikina.

“Albino ni ulemavu ambao mtu anakosa aina ya vitamin inayoitwa melaniani…

Inakosekana ikiwemo katika ngozi, nywele na macho” anaendelea kubainisha kuwa: Kuwa albinism ni hali ya kurithi kutoka kwa wazazi wote wawili ama mmoja. Ni kwamba baba na mama wanakuwa na vinasaba vinavyokuwa na albinism na vinapokutana wakati wa kutunga mtoto ndipo mtoto mwenye albinism anazaliwa.

MO DEWJI BLOG: Vipi inahusishwa na suala la Imani?

DK. POSSI: “Imani sio dini, Ni imani ya kishirikina.

“Sijui kitu gani ambacho kimetokea kikaleta hiyo imani, kwa kifupi ipo kwenye jamii iliyoendelea na uwezo wake wa kiuchumi ni mdogo na elimu pia.

Pia tunaweza kusema: “Suala hili ni la imani, Imani si ya dini, bali ni ya kishirikina. Kwa sababu kuna mtu anasema yeye muislamu ama mkristo.

Au kuna mtu ana Phd/ Profesa, ama amesoma elimu nzuri tu ama ana pesa anafanya biashara au mfanyabishara au mwanasiasa mwenye elimu yake nzuri lakini ametumbukia kwenye imani hii ya kishirikina.

DSC_0355

Mwanadishi wa habari wa modewjiblog, Andrew Chale akiwa kwenye mahojiano maalum na Dk. Ally Possi.

MO DEWJI BLOG: Kwa nini Kanda ya ziwa mauaji haya yamezidi kwa kasi?.

Dk. POSSI: “Kwanza kuna tatizo: Ofkozi..mauaji hayo Kanda ya ziwa mauaji yameripotiwa sana pia kuna Morogoro pia na sehemu nyingine.

“Serikali imekuwa kimya sana… katika mauaji yametokea husikii kiongozi mkubwa, ukiondoa Rais alivyosema (Machi 2-wakati wa hotuba ya mwisho wa mwezi wa Februari), lakini kiongozi mkubwa wa juu Waziri Mkuu, tangu mtoto Yohana  yule wa Geita, Chato kukutwa ameuwawa

Sijasikia kauli nyingine zaidi ya Rais…Ambayo nayo ameitoa wiki mbili hadi moja na nusu, kupita ndio Rais anatoa tamko hilo.

“Nafikiri Serikali  imekaa kimya kutoa matamko ama imekuwa ‘slow’ kuchukua maamuzi ama hatua stahiki hasa kwa watuhumiwa huko vijijini.

“Sote tumekaa vijijini ama tuna ndugu vijijini, Mtu anaweza kuibaa Baiskeli kijijini lakini masaa tu, anakamatwa. Lakini  watuhumiwa wale wa vijiji wa mauaji ya watu wenye albinism kwa nini ichukue muda wasikamatwe?.

MO DEWJI BLOG: Tuambie inakuaje katika suala la kisheria?.

Dk. POSSI: “Sidhani kama kuna kitu kigumu kuwachukua watuhumiwa vijijini, wakati mtu akiiba baiskeli baada ya muda anakamatwa. Hapa nadhani suala la kisheria lipo kwa watu wote. Sheria inabidi ichukue mkondo wake kwa kuchukua maamuzi stahiki na ya haraka katika kuyafanyia kazi ikiwemo kuwakamata watuhumiwa popote walipo.

DSC_0375

Dk. Ally Possi akiendelea kufungua wakati wa mahojiano maalum ndani ya ofisi za modewjiblog jijini Dar es Salaam.

MO DEWJI BLOG: Je? Sheria inasemaje kwani watu mbalimbali wenye uchungu na jambo hili ikiwemo wanaharakati, Wanataka  wale wote wanaokamatwa na viungo!, Wanyongwe ama wapewe adhabu kali?. Hili unalizungumziaje ukiwa Mwanasheria na kwa upande wako wewe kama wewe maoni yako?.

Dk. POSSI: “Kisheria kwanza mtu akikamatwa sheria haisemi anyongwe. Adhabu ya kunyongwa ni ya mtu kuuwa kwa kukusudia na mahakama ndio inaamua.

Kuuwa kwa kukusudia mahakama ndio itaamuru mtu anyongwe na hapo hapo Rais atabidi asaini.

..lakini pia, kwa kunyongwa, Mimi sioni ni suluhisho. Watu wanafungwa miaka 30, kwa kubaka,Lakini bado watu wanabaka wanaendelea kubaka wakati adhabu hiyo kali ipo na tatizo lipo.

“Mimi naamini. Tatizo ni la kwenye jamiii kuwa na imani potofu. Jamii inabidi ielewe kufanya kazi  kwa bidii na kupata elimu bora, Ndio mtu utafanikiwa na si kwa ushirikina..”. anasema Dk. Possi.

Dk. Possi anabainisha kuwa,  endapo tutashindwa kukomesha kwa haraka na kwa kushirikiana juu ya mauaji haya kwa watu wenye albinism, Inaweza ikawa watu hao wenye kufanya vitendo hivi, kesho  wakahamia kwa Bibi mwenye macho mekundu kama tunavyoshuhudia katika baadhi ya mikoa ,ama bibi mwenye miaka 30 au Mtoto mchanga aliyezaliwa tu Pwani ama Zanzibar au kwingineko!.

MO DEWJI BLOG: Watu wengi wanataka Rais asaini adhabu ya kifo. Unalizungumziaje hili kwa upande wako?.

Dk. POSSI: “ Ni kweli pia kuna wengine wanajiuliza kwa nini Rais asaini hiyo adhabu ya sheria ya kifo?..

Siku hizi pia kuna mambo ya haki za binadamu, kuna protocol ya Human Rights  ya kimataifa, namba 2, hiyo protocol Tanzania hatuja saini, inamaanisha tunaweza Tanzania tukapinga ama la!.

“Hiyo protocol inasema nchi ikatae sheria ya kifo, nchi zipinge, kwani hukumu za kifo sio haki kwa binadamu, mimi mwenyewe pia sikubaliani na hiyo adhabu ya hukumu ya kifo. Inaonekana si haki ya mwanadamu.

MO DEWJI BLOG: Unafikiri ni adhabu gani ichukuliwe/ kitu gani kifanyike dhidi ya wahusika wa vitendo hivi?

Dk.POSSI: “kwanza mimi nafikiri hatua ambayo haijachukuliwa ni kuwakamata hawa watu wanaohusika na hivi vitendo.

Pili  hata kama wamehukumiwa kunyongwa basi wahukumiwe…. lakini  hawajahukumiwa in the first place. Hiyo tu inafanya wale wanaofanya hayo mambo  kuendelea kuona kwamba hakuna hatua yoyote yanayofanywa dhidi yao”.

DSC_0290

Mahojiano yakiendelea.

MO DEWJI BLOG:  Kwanini hawajahukumiwa?.

Dk. POSSI: “Waliohukumiwa ni wachache hawafiki watano.. zimeripotiwa vifo zaidi ya 70, hivyo tu vimeripotiwa pekee.

Lakini kuna vifo na matukio zaidi ya hayo ambayo hayajaripotiwa na kutakuwa tu zaidi ambayo hatuyajui.!..

Dkt. Possi anabainisha kuwa,  kuna taarifa zingine mtoto anazaliwa, lakini mama anaambiwa mtoto amekufa, Ilimradi tu imani potofu ikiwemo suala la kuona mkosi katika jamii inayowazunguka hasa vijijini.

“Vijijini huko ukiwa mlemavu wa aina yoyote tu unatengwa ama unauwawa. Vijijini ukiwa na utofauti kidogo tu, unatengwa ama unauliwa.

“Mfano nakumbuka nilipokuwa nasoma Afrika Kusini haya mambo yangu ya sheria, tuliwahi kuishitaki Nigeria kimataifa kwa kutokana na kuuwa watu walioonekana wamezaliwa na hali tofauti na jamii ya wengine ‘abnormal’  yaani watu wafupi, tulifuatilia kesi ile na tukaweza kuishitaki nchi kama nchi katika mahakama ya kiuhalifu ya Arusha na tuliweza kukomesha mauaji yale.

MO DEWJI BLOG: Je unahisi serikali jambo hili haliichukulii kwa dhati ama?.. Ikumbukwe, Waziri Mkuu aliwahi kulia Bungeni?.

Dk. POSSI: “Kwanza Waziri Mkuu kulia yeye ni binadamu, Rais pia alilia kwa Capt. Komba, Pia wanasiasa walilichukulia kulia kwa Waziri Mkuu..waliliweka kisiasa zaidi.

Yule ni binadamu. wabunge kwanza niliwashangaa sana siku ile, baada ya kusema Waziri Mkuu umeteleza, wao walitumia statement ile ile kumbana Waziri Mkuu..

Wauwawe, wao baada ya kusema Waziri Mkuu umeteleza, wakaanza kumbana wazirii mkuu.

Lakini Wabunge  hasa wabunge wa upinzani hawaibani Serikali katika hili la mauaji ya watu wenye albinism kama katika mambo mengine ya kisiasa.

Wabunge hao hao mauaji yanatokea leo, wabunge wa upinzani hawasusi, hawatoki bungeni wala kuibana serikali ama kuandamana.

MO DEWJI BLOG: Nani wa kulaumiwa?

Dk. POSSI: “Serikali itabidi ilaumiwe kwa sababu, Mauaji bado yanaendelea. Ukatili unaendelea, Kwa hili haiepukiki kulaumiwa” Alifafanua Dk. Possi.

MO DEWJI BLOG: Watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, wanaharakati na wengineo, wanataka wenye albinism, waombewa hifadhi ama kutengewa maeneo maaalum, Unalizumziaje hilo?

Dk. POSSI: “Kutengewa maeneo maalum sio suluhisho. Kwanza ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kila binadamu ana haki ya kuishi katika jamii unapomtengea unambagua. Hata katika elimu, kuna mambo mengi sana yameainishwa dhidi ya watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu, hivyo endapo itafanyika hili litawaathiri sana watoto walemavu.

Dkt. Possi anabainisha kuwa, ukimtenga, baadae anaporudi kwa jamii itachangia unyanyapaa. Hii ni tatizo kubwa sana, nitaishauri serikali kama ina mpango huo isifanye hivyo.

“Pia nasikia Waziri Mkuu anataka kufanya hivyo, ninamshauri kuacha zaidi wasimamie kwenye kutoa elimu sahihi ya kupambana na hili.

DSC_0308

MO DEWJI BLOG: Jamii unaiambiaje? Wakiwemo viongozi wa dini, siasa na serikali?

Dk. POSSI: “Viongozi wa dini watoe elimu kwa waumini wao, kuwa maendeleo yanapatikana vipi.

Kwa kujituma na kwa kufanya kazi kwa bidii. hivyo wafanye kazi yao kwa kuelimisha, pia wasiingie kwenye masuala ya siasa.

Dk. Possi anabainisha kuwa:  “Mfano mzuri watu wa dini walisigana wakati wa tukio la kikombe cha babu, ambapo viongozi hao wa dini walimtetea babu wengine wakapinga..

Hili ni miongoni mwa jambo la kishirikina, watu waliamua kuacha dawa na kukimbilia huko matokeo yake wengine wakapoteza maisha, sasa serikali ikakaa kimya hapo hapo unadhani unamsikia mtu yoyote anaenda kwa Babu kunywa dawa? Babu si yupo? Na watu wanazidi kufa ..

Hii ndio tunasema imani, yani endapo jamii itapewa elimu ya kutosha imani hizi  potofu ili kuondolewa basi tutapiga hatua na kupambana.

Dkt. Possi anabainisha kwa kina juu ya viongozi wa siasa: Viongozi wa siasa nao rahisi kutupiwa lawama kwani hawagomi, hawatoi tamko lolote kuitisha mikutano na kadhalika, lakini ikifika wakati wa kuomba kura kwenye kampeni ndio wanatukumbuka kwa kutuhubiria maneno mazuri.

MO DEWJI BLOG: Bila shaka jamii itakuwa inaendelea kupata mwanga wa jambo hili hasa kwa jamii kuendekeza imani potofu.

Dk. POSSI: “Ni kweli jamii ielewe kuwa, Chanzo ni imani potofu. Hivyo hawana budi kuachana nazo imani hizo kwani si za kweli na zinarudisha maendeleo nyuma.

Jamii ambayo inaelekea kushindwa, ndio yenye kufanya vitu vya kikatili na kuendeleza imani hizi.

“Ukimuona yule mama alivyojeruhiwa, hapa sasa ni suala la ubinadamu kwani huwezi kumjeruhi mtu namna ya yule mama.

MO DEWJI BLOG: Labda mbali na matukio haya. Changamoto zingine ni zipi zinazowakabili?

Dk. POSSI: “Changamoto ni nyingi, ikiwemo suala la unyanyapaa. Pia tatizo kubwa sana ni la macho linawakumba walemavu wengi wa ngozi. Ni wengi wao wanasumbuliwa na tatizo la macho ikiwemo kutoona vizuri.

Hivyo mtoto anaweza asiweze kusomaa vizuri na wenzake awapo darasani.

Pia familia nyingi za albinism zinanyanyaswa, kuteswa katika familia na mambo mengine mengi, Kinachohitajika ni kutolewa elimu sahihi kwa jamii yote.

Dk. Possi anabainisha kuwa, Wapo wanaofariki kwa tatizo la macho, kansa ya ngozi na mambo mengi.

DSC_0392

MO DEWJI BLOG: Vipi kuhusiana na chama cha Watu wenye albinism (TAS)?.

Dk. POSSI: “Kuna mambo mengi yanahitajika kwa sasa kwa kuwa tupo inabidi tuendelee kusaidia katika hili ikiwemo kukijengea uwezo.

Chama kinahitajika kutoa elimu ya kutosha ambapo serikali inatakiwa kuwapiga tafu kwa namna yoyote ile na wala si kuwategemea wasaidiwe na wafadhili wa nje?.

Wasaidiwe watendaji kazi  kwani waliopo ni wachache hivyo  wanahitaji kusaidiwa na kuwezeshwa pia  kwa kila msaada.

Pia naweza kusema kuwa,  Serikali inachelewa pia kuandaa chaji za kesi za watu wanaotuhumiwa kutesa na kuua albino.

Watuhumiwa wengi wanashinda kesi.. Ikichangiwa na suala la rushwa kwani pia linachangia kwani wapo baadhi ya watuhumiwa wanahonga pesa na wanaachiwa/wanashinda kesi.

MO DEWJI BLOG: Vipi mipango yako kwa sasa?.

Dk. POSSI: “Mimi ni mwanasheria na mhadhiri wa chuo. Pia katika hili la sasa nipo katika kuandaa program maalum ya juu ya kupambana na mauaji ya watu wenye albinism ambayo nitaiandaa kisheria.

Dondoo za Dk. Possi.

Ambapo anaeleza kuwa,  vitendo vya kikatili na kuuwa ni imani potofu ambayo imeingia katika jamii. Chanzo kikubwa ni kufeli kwa mtazamo wa kijamii hasa watanzania.

Dk. Possi ni mlemavu wa ngozi, ni msomi mwenye elimu ya Uzamivu ( PhD) na wakili wa kijitegemea.

Dk. Possi anabainisha kuwa, jamii inayoamini katika ushirikiana haiwezi kuendelea, na kwamba ili kumaliza tatizo hilo, ni lazima kujua jamii ina tatizo gani.

 Dk. Possi anaamini,  Serikali ikichukua hatua madhubuti na vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali jambo hilo linaweza kukoma kabisa.

“Tuwe na jamii inayoamini kuwa elimu na kufanya kazi kwa bidii, ndiyo italeta maendeleo,” alibainisha Dk.Possi.

DSC_0304

MO DEWJI BLOG:  Dk. Possi ni nani?

Dkt. Ally Possi ni kaka wa Dk. Abdallah Possi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma ( Udom).

Mama yao ni Profesa anafundisha Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku baba yao ni mstaafu.

 Dk Ally Possi, alipata elimu yake ya  shule ya msingi Olympio, Upanga Jijini Dar es Salaam hadi mwaka 1998 na kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Makongo mwaka 1999.

Hapo, alisoma kidato cha kwanza hadi cha sita baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2005 hadi 2008 na kutunukiwa Shahada ya Sheria.

Mwaka 2009 hadi 2010 anasema kuwa alipata Shahada ya Uzamili ya sheria katika Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini (UCT). Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Pretoria na kutunikiwa Shahada za Uzamivu (PhD).

Kwa sasa yeye ni mtaalamu wa sheria na wakili wa kijitegemea.

Pia ni mtaalamu wa sheria za kimataifa (International law).

“ Nilichokiona  ukiwa mashuleni ni ile ‘impression’ (mtazamo ) mtu akikuona kuwa ni Albino anakuogopa. Hata marafiki niliokuwa nao, lakini sio wengi wanakuona kuwa huwezi na wakati mwingine hawataki kukugusa,” anafafanua.

 >>> Tunashukuru kwa kuperuzi Mo dewji blog hakika endelea kuwa nasi kwani kila siku tutakuletea makala maalum na habari moto moto na za kina.

Pia waweza kutoa maoni yako kupitia blog hii ama simu namba 0719076376


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles