Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura.
Katika kile kinachoelezwa kitendo cha kikatili, dhidi ya watoto kushamiri, Mtoto wa mwaka mmoja na miezi sita (jina limehifadhiwa ),anadaiwa kuteswa na mama yake mzazi kwa kipindi cha miezi kumi akiwa amefungiwa ndani huku akila magodoro baada ya kubainika na majirani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Neema Brian wa mtandao wa http://sautiyamnyonge.com alibainisha kuwa, Mtoto huyo ambaye amelazwa katika hospitali ya Mwananyamala, ambaye analelewa na mama yake mzazi, aligundulika na majirani wa familia yake katika Mtaa wa Msisiri A Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Majirani waligundua tukio hilo baada ya kusikia sauti ya mtoto huyo akilia ndani ya chumba alichokuwa anaishi mama mzazi pamoja na familia yake katika mtaa huo.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msisiri A, Juma Mbena, alisema tukio hilo lilitokea jumapili ya wiki iliyopita, baada ya majirani kusikia kilio cha mtoto mdogo ndani ya nyumba anayoishi mama mzazi wa mtoto na bibi yake kwa muda mrefu.
“Wananchi walifika hapa kutoa taarifa za kuwepo kilio cha mtoto ndani ya nymba tuliamua kwenda kutoa ripoti Jeshi la Polisi ili tuweze kuvunja mlango,lakini tuliporudi tulikuta wananchi wamevunja mlango na kumtoa mtoto huyo ambaye alikuwa katika hali mbaya sana”alisema Mbena.
Alisema baada ya wananchi kuvunja mlango walimtoa mtoto huyo akiwa mwenye njaa kali huku akiwa amechafuka kinyesi kutokana na kutosafishwa na mzazi wake huyo.
Aliongeza “polisi walifungua kesi yenye namba OB/RB/3199/2015,nakufanikiwa kumkamata mama mzazi wa mtoto akafikishwa kituo cha polisi cha Oysterbay kwa maelezo zaidi.”
Baadhi ya majirani wakielezea tukio hilo, walisema katika chumba hicho kunaishi watu watano ikiwa ni bibi wa mtoto Sofia Abasi Nyangasa(40),mama wa mtoto Swaumu Hamis(23), watoto wengine wawili ikiwa ni pamoja na mtoto aliyeteswa.
Abduli Mushi jirani ya mama huyo alisema”tabia ya mama huyu sio nzuri hata kidodo kwani amekuwa na matusi sana mwanzo alikuwa na mtoto mchanga lakini alikufa inaelekea nikutokana na tabia hii ya kutesa watoto,” alisema na kuongeza:
“Akiamua kumpiga mtoto anachukua kisu na kupasha moto kisha anamchanja chanja mtoto kama kitunguu bila hata kujali umri wa mtoto,”
Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba hiyo Luka Mbapila, ambaye alimfadhili mama huyo kutokana na mafuriko ya mvua yaliyotokea mwaka jana, alisema hakufahamu kama mama huyo ni katili kiasi hicho. Mbapila, ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mtaa wa Msisiri A, alisema chama kilimpa hifadhi ya nyumba kutokana na nyumba yake kuzolewa na mafuriko.
Mbapila alisema “huyu mama tulimpa hifadhi hapa kwetu baada ya kuja kwetu kuomba tumsaidie,lakini hatukujua kama anaukatili huu kwa kiumbe cha Mungu.”
Alisema wao kama chama, wanalaani vikali kitendo kilichofanywa na mzazi huyo ambae hana sifa ya kuitwa mzazi.
Afisa Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Mwananyamala, Rozi Temu, alisema kwa sasa mtoto huyo anaendelea vizuri ila kinacho msumbua ni utapia mlo na majeraha aliyokuwa nayo.
Mtandao huu wa Modewji blog utaendelea kukujuza tukio hili juu ya maendeleo ya mtoto kadri ya uwezo wetu. Endelea kufuatilia.
