Mkurugenzi mtendaji TASAF, akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kazi kilichohudhuriwa na waratibu wa mpango, wahasibu wa mpango, maafisa ufuatiliaji na baadhi ya waandishi wa habari kutoka mkoa wa Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jeshi la magereza,Umwema mjini Morogoro.Kulia ni Mkurugenzi wa uratibu TASAF, Alphonce Kyanga na kushoto ni Mkurugenzi wa kujenga uwezo wa TASAF, Fariji Mishael.
Na Nathaniel Limu, Morogoro
WAANDISHI wa habari nchini,wamehimizwa kufanya kazi kwa karibu zaidi na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF),ili pamoja na mambo mengine,kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna bora ya kutumia mfuko huo kuondoa umaskini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga, wakati akifungua kikao cha kazi kilichohudhuriwa na waratibu, wahasibu wa mpango, maafisa ufuatiliaji na baadhi ya waandishi wa habari kutoka mkoa wa Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa jeshi la magereza mjini hapa.
Alisema wananchi wengi na hasa wale waishio katika maeneo ya vijijini, hawana elimu ya kutosha juu ya shughuli zinazotekelezwa na TASAF, kitendo kinachochangia iwe rahisi kwao kupotoshwa.
Baadhi ya wadau wa TASAF kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro na Pwani, waliohudhuria kikao cha kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jeshi la magereza mjini Morogoro.
“Baadhi ya watu wasioitakia mema TASAF, wamekuwa wakieneza sumu au upotoshaji kwa lengo la kukwamisha juhudi za mfuko wetu kuwahudumia walengwa kwa ufanisi.Watu hao wamefika mbali zaidi kwa kuipotosha jamii eti fedha za TASAF zinazotolewa kwa kaya maskini, ni za ‘freemason'”, alifafanua Mkurugenzi huyo.
Mwamanga alisema kuwa ili kuzima juhudi hizo zinazofanywa na baadhi ya watu kupotosha wananchi, waandishi wa habari wanalo jukumu kubwa la kutumia kalamu zao kuielimisha jamii juu ya malengo ya mfuko huo na kwamba mfuko huo ni mpango wa serikali na sio NGOs kama watu wengi wanavyofikiria.
Aidha, amewataka pia wahakikishe wanatoa msukumo kwa serikali na vyombo vyake kuwatumikia wananchi ipasavyo. Kwa upande wa vyombo vya habari, navyo vithibitishe wazi kwamba ni kweli vipo kwa niaba ya sauti ya wanyonge kwa kuibua kero mbalimbali zinazowasibu.
“Nawaomba waandishi wa habari, jengeni utamaduni wa kutembelea maeneo ya vijijini ili muweze kuibua kero au mapungufu kama yapo ya mfuko wetu. Mkifanya hivyo mtatusaidia kuboresha utendaji wetu wa kusaidia jamii kuondokana na umaskini”, alisema.
Kwa upande wa TASAF, Mkurugenzi huyo amewataka watendaji/watumishi wake watoe ushirikiano wa dhati kwa waandishi wa habari,ili waweze kufanya kazi yao vizuri ya kuelimisha jamii juu ya shughuli zinazotekelezwa na mfuko huo chini ya mpango wa kupunguza umaskini.
Mkurugenzi mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga (wa tatu kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na waratibu wa mpango wa TASAF wa kupunguza umaskini kutoka mkoa wa Singida,Wengine ni wahasibu wa mpango,wafuatiliaji na baadhi ya waandishi wa habari.
Jengo la ukumbi wa mikutano wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro mahali kikao cha kazi cha mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kilichomalizika jana mjini Morogoro.(Picha zote na Nathaniel Limu).




