Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti.
Na demasho.com
Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imefanya tathimini ya elimu ya na matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2014 katika ukumbi wa EMAU Peremiho.
Katika tathimini hiyo mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti amewataka Madiwani ,Maafisa tarafa, Watendaji wa kata na Watendaji wa Vijiji kuwapa elimu wazazi juu ya umuhimu wa kuchangia chakula cha kutosheleza muhula wa masomo ili kusaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo.
“Kwani kufanya hivo kutasaidia wanafunzi kujifunza muda wote wawapo shuleni na kujenga ushirikiano baina yao wanapokuwa pamoja na hali hiyo itainua kiwango cha ufaulu” alisema Mkirikiti.
Hata hivyo Mkirikiti amewataka Madiwani, Maafisa tarafa, Watendaji wa kata na Watendaji kuacha kusingizia wanasiasa kuwa wamezuia suala la kuchangia chakula
“ Tabia ya kuwasingizia wanasiasa kuwa wamezua kuchangia chakula mashuleni muache sio kila kitu kusingizia wanasiasa hivi ni kiongozi gani asiependa maendeleo ?, maana hivi sasa kila kitu wanasiasa wamezuia hasa kipindi hiki tunachoenda cha uchaguzi utasikia wanasiasa wamezuia ukiona mwanasiasa anazuia basi huyo ni SHIDAAA ”Alisema Mkirikiti.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea vijijini – Sigsibert Valentine akitoa hoja katika tathimini ya elimu kwa Halmashauri yake ya Songea Vijini.
Naye Kaimu Afisa elimu wilaya Bw. Tanu Kameka ameomba baada ya Tathimini hiyo wakutane na waratibu wakata, wazazi, walimu pamoja na watendaje ili uongezwe muda wa ziada wa ufundishaji ili kuweza kuleta mwamko wa elimu katika halmashauri hiyo ya Songea vijijini na kuleta ufaulu mzuri.
“ Miaka yote tumekuwa tukifanya hivo na ndiyo maana tukawa tunaongoza katika matokeo , ila kwa mwaka jana hatukuweza kusimamia hili swala la muda wa ziada ndiyo maana tumeshuka ila kwa mwaka huu tunalirudisha swala la muda wa ziada hivyo tutafanya vizuri katika matokeo” Alisema Bw. Kameka.