Makamu wa Rais wa Tanzania, Dr. Mohamed Gharib Bilal.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dr. Mohamed Gharib Bilal ataungana na taasisi ya ONE pamoja na Restless Development katika majadiliano na vijana walio na miaka 15 ikiwa na lengo la kuwapa nafasi vijana kutoa mawazo yao kwa watunga sera namna ambavyo wanatarajia vipaumbele vyao vya maendeleo viwe ili wawe na ustawi mzuri ifikapo mwaka 2030.
Majadiliano hayo ambayo ni sehemu ya ‘action2015’, ikiwa ni msukumo kutoka kwa wananchi unaoendeshwa na taasisi zipatazo 1000 duniani kote ina lengo la kukuza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa mwaka 2015 na pia kutoa mahitaji yanayotekelezeka kumaliza umaskini na ukosefu wa usawa duniani.
Wawakilishi wa vijana waliochaguliwa kutoka sehemu zote za Tanzania watashiriki katika majadiliano hayo yatakayofanyika katika hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam, na vijana watapaza sauti zao kutaja vipaumbele vyao kuelekea mikutano ya viongozi wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015 kupanga vipaumbele vya maendeleo.
Mwaka 2015 ni mwaka wa kipekee kwa viongozi wa dunia kupanga mikakati kuelekea kumaliza umaskini uliokithiri, magonjwa yanayotibika, kumaliza vifo vya watoto katika upangaji wa vipaumbele vya dunia kuelekea 2030, ambavyo vitavibadilia hivi vya sasa 2000-2015.
Akizungumza kuhusu majadiliano hayo, Oscar Kimaro wa Restless Development alisema vijana Tanzania wanajumuisha karibu asilimia 60 ya wakazi wote, wakati wale walio na miaka 15 sasa walizaliwa wakati vipaumbele vya 2000-2015 vinazinduliwa.
‘’Baada ya mwaka 2015 ajenda kuu ya maendeleo ni kujenga ustawi mzuri kwa vijana, ambao watakuwa na miaka 30 wakati vipaumbele hivi vinamaliza muda wake. Hawa ndio wanaotarajiwa kuwawajibisha viongozi wetu kwa maamuzi yatakayopitishwa mwaka huu hivyo sauti zao na ushiriki wao ni muhimu sana’ alisema Kimaro.
Majadiliano hayo pia yanatarajiwa kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Mkurugenzi Mkuu wa ONE Africa, Dr Sipho Moyo, mabalozi wa ONE Tanzania, Diamond Platnumz na AY, pamoja na viongozi wengine wa serikali na asasi za kijamii.
Majadiliano hayo yatarushwa moja kwa moja katika kituo cha luninga cha Clouds TV na washirika wataweza kushiriki kwa kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.
Ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya ‘action2015’, nchi zaidi ya 50 duniani zinafanya majadiliano kama haya, mojawapo ya nchi ni South Africa, Liberia, Nigeria, Lebanon, Norway, the United Kingdom, USA na Sri Lanka