Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda (pichani) amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuendesha kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na kuepuka maneno ya uchochezi.
Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wananchi ambao hawajajiandikisha katika Rejesta ya Wapigakura kufanya hivyo bila kukosa kutokana na kuonekana wengi hawajajiandikisha hadi sasa.
Pinda alitoa rai hiyo jana wakati akihitimisha shughuli za mkutano wa 16 na 17 wa Bunge ambapo bunge hilo limeahirishwa hadi Januari 27 mwakani.
“Napenda nitumie nafasi hii kutoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa waendeshe kampeni kwa amani na kuepuka maneno ya uchochezi, kubaguana kwa misingi ya ukabila, rangi, udini ama hali ya mtu, mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.”
“Nawaomba viongozi wa vyama vya siasa na wanachama wao, wakishapiga kura (kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa) wasiendelee kukaa katika vituo vya kupigia kura, bali watawanyike na kusubiri muda wa matokeo,” alisema.
Ili kufanikisha uchaguzi huo, alisema masanduku ya kupigia kura yameshanunuliwa na tayari yameshasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara.
Alisema Serikali imekwishaandaa na kuchapisha vipeperushi, fomu za wagombea, rejesta ya wapigakura, karatasi za kuonesha vituo vya kupigia kura, mabango na matangazo mengine kuhusu elimu kwa mpiga kura na kusisitiza “Tayari vifaa hivyo vimepelekwa mikoani na vingine vinaendelea kupelekwa”.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wasimamizi wa uchaguzi wahakikishe vifaa vya uchaguzi vinafika kwenye maeneo yao kwa wakati.
Alisema jumla ya vijiji 12,443, vitongoji 64,616 na mitaa 3,741 vitahusika katika uchaguzi huo utakaofanyika Desemba 14 mwaka huu.
Uchaguzi huo unahusisha Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu ameahidi serikali kutekeleza ushauri wote uliotolewa na wabunge wakati wa kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016.
“Maoni na Ushauri tuliopokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge tutauzingatia wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2015/2016. “ alisema Waziri Mkuu.
Katika Mpango huo wa Maendeleo uliosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 5.8 kwa utekelezaji wa mpango huo.
Wasira alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/2016 utagharimiwa na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na mapato ya ndani, misaada pamoja na ushiriki wa sekta binafsi.
Alisema Serikali itakopa ndani na nje ya nchi hususan mikopo yenye masharti nafuu kwa kuzingatia ukomo wa uhimilivu wa deni la Taifa, ili kufanikisha utekelezaji wa miradi.
Katika bajeti ya maendeleo 2015/2016, Serikali itatenga Sh trilioni 5.7 ili kutekeleza miradi ya maendeleo, ambapo fedha za ndani zitakuwa Sh trilioni 3.27 na fedha za nje Sh trilioni 2.5.
Aidha katika mpango huo Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ili kuwezesha sekta binafsi kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakichangia mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa sekta hiyo, David Silinde walizungumzia ukubwa wa matumizi ya Serikali ukilinganisha na mapato, wakiitaka Serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuchochea maendeleo.
Miswada iliyopitishwa ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014; Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani wa Mwaka 2014 ; Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 ; na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014.
Aidha Miswada 11 ya Sheria ya Serikali kuhusu mambo mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.
Mkutano huo wa 16 na 17 ambao ulivuta hisia za wengi kutokana na shauri la akaunti ya Escrow Tegeta, wabunge walipata pia fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na waheshimiwa wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, maswali 18 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Pamoja na maswali hayo pia Bunge lilisikiliza na kuridhia kauli mbalimbali za serikali ikiwamo ya mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto.
