Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria, amesema taasisi hiyo imesikitishwa na taarifa kuwa vituo vya kutolea huduma ya afya nchini vinakabiliwa na uhaba wa dawa na vifaatiba.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kiria, alisema upungufu huo unasemekana umekuwa ukiwaathiri zaidi wananchi wasiokuwa na bima za afya.
Alisema uhaba huo wa dawa na vifaatiba muhimu unaondelea ulitokana na Bohari Kuu ya Taifa (MSD), kusimamisha kutoa huduma katika vituo hivyo, hadi pale serikali itakapolipa mlundikano wa madeni inayodai.
Alivitaja vituo vilivyokumbwa na kadhia hiyo ya kukosa huduma ya MSD kuwa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hospitali za wilaya za kiteto, Mpwapwa na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa Sikika pamoja na vyombo vya habari, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa zaidi y ash bilioni 90 ambazo ni gharama ya ugomboaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa kutoka miradi misonge.
Baadhi ya vituo vingine vyenye madeni ni Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo inadaiwa sh bilioni nane, hospitali ya wilaya ya Kiteko sh milioni 38, na nyingine.
Kiria alisema ongezeko la deni kwa MSD limekuwa likiathiri ufanisi wa bahari hiyo kutokana na ukweli kuwa hifanyi kazi kwa faida na mtaji wa kujiendesha yenyewe umekuwa ukipungua siku hadi siku.
Alisema hali hiyo inasababisha ishindwe kufanya manunuzi kwa wakati, kusambaza na kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaatiba.
Aidha, asilimia 80 ya watanzania hawako katika mfumo wowote wa bima za afya na inapotokea uhaba wa dawa na vifaatiba, wamekuwa wakiathirika kwani inawalalizimu kununua dawa kwa gharama kubwa wakati mwingine hukosa kabisa
“Hali hii huathiri utaratibu wa matibabu yao na kusababisha matabaka kati ya wale wasio nacho na walio nacho kwani walio nacho wamekuwa wakipata huduma za afya,”alisema Kiria.
Kutokana na hali hiyo Sikika inapendekeza serikali itimize ahadi ya kutoa fedha zote za dawa na vifaatiba muhimu na zitolewe kwa wakati sahihi.
Aliongeza kuwa serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii iongeze idadi ya watu katika mfuko wa bima ya afya (NHIF), ili liomgeza mapato.
Alisema hiyo itawezesha kulipia huduma hata kwa wale wachache watakaoshindwa kujiunga na mifuko ya bima za afaya.
Kiria alisema ni wakati kwa MSD kutimiza mahitaji ya dawa katika vituo kwa asilimia 100 hali itakayosaidia vituo hivyo kuendelea kutoa huduma wakati wa uhaba kwani watakuwa wanatumia akiba waliyonayo.