Na Mwandishi wetu
IDARA ya Uhamiaji inaanza msako wa nyumba kwa nyumba kubaini wahamiaji haramu kwa kuchukua taarifa za wanandoa ambao wameolewa na raia wa kigeni ili kubaini wahamiaji hao.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Okororo, kwenye semina ya siku moja kwa Maafisa Watendaji wa Mtaa wa Wilaya ya Ilala, iliyofanyika ukumbi wa Korea Jijini Dar es Salaam.
Okororo alisema, kwa muda mrefu sasa wageni hususani wanaume kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakitumia mgongo wa kuoa wanawake wa Tanzania ili kuweza kujipatia hifadhi.
Alisema wameamua kushirikiana na maafisa watendaji wa mitaa kutokana na kuwa karibu na wananchi.
“Kisheria mtu yoyote mgeni anayeingia nchini anatakiwa kutoa taarifa kwa Mtendaji wa Mtaa lakini hilo kwa sasa halifanyiki jambo linalochangia ongezeko la wahamiaji haramu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu,” alisema.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhandisi Raymond Mushi, alikiri kwamba watendaji wamekuwa hawalipi kipaumbele suala la wahamiaji katika shughuli zao za kila siku.
Mushi alisema anaamini kwamba kila Mtendaji akitekeleza wajibu wake ikiwemo kujitathimini kila siku ana imani suala la uhamiaji haramu litapungua ama kuisha kabisa.
Aidha Naibu Kamishna Uhamiaji, Wilaya ya Ilala, Safina Muhindi alisema, jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na wageni wengi kutokana na kuwa kitovu cha shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, shughuli za kitalii, uwekezaji, diplomasia na masomo.