Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Edward Ole Lenga.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Mkalama
SERIKALI wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida, imeishukuru serikali kuu kwa hatua yake ya kuipatia huduma ya nishati ya umeme kwa kipindi kifupi mno.
Shukrani hizo zimetolewa na mkuu wa wilaya hiyo, Edward Ole Lenga wakati akizungumza na Mwakilishi wa MOBlog, juu ya maendeleo ya usambazaji wa huduma hiyo ya umeme kupitia matokeo makubwa sasa (BRN)katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.
Akifafanua,alisema kazi ya kusimika nguzo kuanzia kijiji cha Iguguno mahali umeme wa grid ya kitaifa unapita, hadi Nduguti, makao makuu ya wilaya imefanyika kwa kipindi kifupi mno.
“Kutokana na kasi hiyo, Oktoba nane mwaka huu umeme katika makao makuu ya wilaya, Nduguti, uliwashwa rasmi. Siku itabaki kuwa historia kwa wakazi wa Mkalama kupata nishati itakayowaharakishia kujiletea maendeleo endelevu”,Lenga alisema.
Akifafanua zaidi, alisema siku umeme unawashwa rasmi,wakazi wa Nduguti walikesha wakifurahia kupata umeme wa grid ya taifa na walisikika wakisema ndoto yao imetimia.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi zake za kuijengea nguvu REA, ambayo inaendelea kwa kasi kubwa kuweka nguzo za umeme kwenye vijiji mbali mbali vya wilaya yetu ambavyo havijapata huduma ya umeme”,alisema.
Aidha, DC Lenga amemshukuru Meneja Tanesco mkoa wa Singida, kwa usimamaizi wake makini, uliowezesha umeme kufika kwa haraka katika makao makuu ya wilaya.
Amemwomba meneja huyo aendelee na kasi hiyo hiyo, ili kufikisha umeme katika vijiji vilivyobaki.
“Pia niwashukuru wananchi wa wilaya yetu kwa kupokea huduma hii muhimu kwa maendeleo yao. Wakazi wengi wa Nduguti wameisha unganishiwa umemme, na mamia ya wakazi wa vijiji mbali mbali vilivyobaki, wameishafanya maandalizi ya kupatiwa nishati hiyo, ili waweze kuitumia kwa maendeleo yao”, alisema Lenga kwa kujiamini.