Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa mkoa wa Lindi kuhakikisha kuwa vijana wao wanaishi maisha ya uadilifu, wanamcha Mwenyezi Mungu na kusoma elimu ya Dunia ili wasipotee katika Ulimwengu wa utandawazi.
Mama Kikwete ametoa wito huo wakati wa futari iliyowajumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa mkoani Lindi.
Amesema kuwa ni jambo jema kwa binadamu kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu, kwani hakuna mtu anayejua siku yake ya kufa, hivo basi ni muhimu kujiandaa mapema kwa kutenda matendo mema ili ukifika huko uwe na mazingira mazuri ya baadaye na hakuna cha kusema kuwa mimi ni mdogo bado, kwani kwa Mungu hakuna cha mdogo wala mkubwa.
Ameongeza kuwa kufunga kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ni lazima, kwani ni moja ya ibada katika kutengeneza afya ya mwili wako na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana hata watoto wadogo wanatakiwa kujifunza kufunga.
Lakini siku hizi kufunga imekuwa ni mtihani kwa baadhi ya watu, kwani kuna wengine wanasingizia ugonjwa ili wasifunge, jambo ambalo si sawa kwa sababu kuna baadhi ya watu wanaugua ugonjwa wa kisukari na wanafunga lakini hawapati matatizo, kwa kuwa ukidhamiria utafunga tu bila tatizo hata kama ni mgonjwa na Mwenyezi Mungu atakupa uzima.
Aidha Mama Kikwete pia amewataka viongozi hao wa Serikali na vyama vya Siasa kutunza amani iliyopo, kwa kuwa amani ni tuzo ya taifa na nchi bila ya kuwa na amani haikaliki na hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika kwani hata wanyama watapata tabu na kukosa mahali pa kuishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila amemshukuru Mama Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa, dini zote zinahimiza umuhimu wa kusali na kutubu hivyo basi ni jukumu la kila mtu kufanya hivyo.
Mkuu wa mkoa huo amesema kuwa kila mtu anatakiwa kumcha Mungu na kumtukuza bila kusahau kuwasaidia watu waliopo katika dhiki, ambao wanatakiwa kusaidiwa kwa kufanya hivyo watapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Naye Shekhe na Kadhi mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani amesema kuwa utaratibu wa watu wa aina mbalimbali kukutana na kufanya jambo kwa pamoja, kunawafanya wapendane zaidi kwani mtu akikupenda nawe utampenda, hivyo basi wawe na mapenzi na kupendana ili wapate raha katika maisha.
Amesema kuwa katika kumi la pili la kufunga ni la msamaha kama alivyosema Mtume Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W), hivyo basi kwa wale wanaofunga wanatakiwa kujikita zaidi katika kufanya mambo mazuri kwa watu ikiwa ni pamoja na kulisha wengine, kwani ukimpa kula na kunywa mwenzako Mwenyezi Mungu anakulipa zaidi.