Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira (pichani), amesema serikali inaandaa sera ya elimu itakayomwezesha mtanzania kujiajiri.
Alisema kuboreshwa kwa sera hiyo kutakwenda sambamba na mitaala inayotumiwa ambayo kwa muda mrefu imeshindwa kumjenga mhitimu katika dhana ya kujiajiri
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akizungumzia mipango ya serikali ya kuinua elimu na kumkomboa Mtanzania katika lindi la umasikini
Wassira alisema sera ya elimu inayotumika ni mwaka 1995 inayohitaji mabadiliko makubwa yatakayomuwezesha mhitimu kuondokana na dhana ya kuajiriwa.
“Dunia ya sasa ni ya Sayansi na Teknolojia watu wetu ni lazima waingie kwenye mabadiliko hayo wakiwa na dhana ya kujiajiri badala ya kuajiriwa,” alisema.
Wassira alisema utawala wa awamu ya nne umetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu ambapo hivi sasa kila kata ina shule ya sekondari.
Alisema mwaka 2004 vyuo vikuu vilikuwa vikitoa walimu 650 kwa mwaka lakini leo hii vinatoa walimu 12,000 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa mwanzo serikali ilipata tabu ya kuamua kati ya ujenzi wa shule au kusomesha walimu lakini waliamua kujenga shule na sasa wamejikita kwenye kuwaongezea maarifa walimu.
Wassira alibainisha uhaba wa ajira ni tatizo kubwa la dunia na Tanzania imeamua kujikita kusambaza elimu ya kujiajiri ili kukabiliana nalo.