Na Mwandishi wetu
MAAMBUKIZI ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwenye vituo vya kulaza magari ya masafa marefu yapo juu kuliko wastani wa kitaifa, mikoa na wilaya husika.
Wastani wa juu wa kitaifa ni asilimia 5.1 na kwenye vituo hivyo maambukizi kwa madereva ni kati ya asilimia 15 hadi 35.
Hayo yalibainishwa na Mratibu wa Programu Maalum kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Renatus Kihingo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema tume kwa kushirikiana na mamlaka ya kudhibiti Ukimwi kutoka Nchi zote kusini mwa jangwa la Sahara, imeanzisha programu ya Vituo vya Maarifa kwa ajili ya huduma ya elimu kwa madereva wa masafa marefu na jamii inayozunguka.
Alisema hadi sasa vituo 14 vimekamilika katika maeneo ya barabara kuu ambapo kati yake vituo nane vya Kongwa na Kibaingwa-Kahama, Kongwa na Mdaula-Bagamoyo, Uvinza na Kazuramimba-Uvinza, Kasulo na Benacco-Ngara vilijengwa chini ya programu ya udhibiti ukimwi ya nchi za Maziwa Makuu.
Alizitaja huduma zitakazotolewa kuwa ni ugawaji wa kondomu, ushahuri nasaha, upimaji wa hiyari, burudani mbadala, rufaa kwa matibabu maalum na ujasiriamali.