Na Mwandishi wetu
WABUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) walio katika kamati ya ya kilimo, Utalii na Maliasili wamekutana kujadili muswada wa sheria ya ushirika wa pamoja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Isabelle Ndahayo, alisema kuwa wamekutana kuupitia muswada wa sheria kuhusiana na vyama vya ushirika ili sheria watakazozipitisha zisaidie vyama hivyo.
Ndahayo alisema kuwa kukutana kwao kutasaidia nchi zilizokatika jumuiya hiyo kwani sheria hiyo ni muunganisho baina ya ushirika na wafanyabiashara ili iwasaidie kushiriki soko la pamoja.
“Tunazunguka maeneo mbalimbali ili kupokea maoni yatakayosaidia kupata sheria nzuri ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ,”alisema.
Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika Nchini (TFC) Hassan Wakasuvi, alisema kuwa muswada huo utawasidia vyama vya ushirika kupata nguvu na kuhakikisha wanapambana na matatizo ya ndani kwani bila ushirika hakuna maendeleo.
Naye Mwakilishi wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Abdullah Makame, alisema kuwa Bunge la Afrika Mashariki litahakikisha linapitisha sheria zitakazowasaidia wakulima wa jumuiya hiyo, kuboresha ushirika ndani ya nchi husika ikiwemo kuhakikisha sheria za ndani zisigongane.