Wakazi wa kaya ya mchungaji Charles Issa Nyambi wa kijiji cha Puma Kituntu wilaya ya Ikungi, wakipura ulezi kwa kutumia fimbo ndefu. Upuraji wa aina hiyo umweanza kupigwa vita na serikali ya mkoa wa Singida kwa madai umepitwa na wakati na pia unachangia nafaka kuwa chafu na zenye mchanga , kitendo ambacho kinahatarisha afya za walaji. (Picha na Nathaniel Limu).
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone ameziagiza halmashauri za wilaya na manispaa ya Singida, kila moja kuangalia uwezekano wa kununua mashine tano za kupura mtama ili kusaidia vikundi vya wakulima.
Dkt. Kone amesema mashine hizo zinazopatikana SIDO mkoa wa Shinyanga, zitasaidia mno wakulima wa mtama na uwele kuondokana na teknolojia duni inayotumika kupura nafaka kwa sasa.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo wakati akitoa mada yake ya kuwawezesha wakulima kupunguza/kudhibiti upotevu wa zao la mtama baada ya mavuno, mbele ya kikao cha wadau wa maendeleo.
Akifafanua zaidi, amesema teknolojia duni zinazotumika kupura mtama ikiwemo ya kutumia fimbo ndefu, inakadiriwa kupoteza asilimia 30 ya mavuno.
Dkt. Kone amesema “Pia upuraji huo wa kienyeji, unachangia mtama/uwele kuwa mchafu na uliojaa mchanga kwa vile unapurwa juu ya ardhi, vile vile miundo mbinu duni ya kuhifadhi mtama/uwele, nayo inachangia upotevu”,
Mkuu huyo wa mkoa, amesema dawa pekee ya kupambana na changamoto hizo ni kuhimiza matumizi ya mashine za kupura mtama, ambazo zinarahisisha kazi ya upuraji, kupunguza upotevu baada ya mavuno na mtama hauwezi kuchanganyika na mchanga.
Amefafanua kuwa “Mtama ulioandaliwa vizuri, utapata bei nzuri sokoni na hivyo kuongeza kipato kwa mkulima na kupunguza umaskini”.
Kwa hali hiyo, amezitaka halmashauri na manispaa ya Singida, kushirikiana na SIDO mkoa wa Singida kuhakikisha mashine hizo zinapatikana mapema iwezekanavyo.
Wakati huo huo, Dkt. Kone amesema elimu ya matumizi mbalimbali ya mtama ikiwemo kutengeneza keki ,wali, mkate na chapati, inaendelea kutolewa kwa kushirikiana na wataalam wa lishe.