Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilal.
Na Rose Masaka, MAELEZO
Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilal anatarajia kuwa mgeni rasmi wa kongamano la wanasayansi vijana duniani linalotajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 11 hadi 14 Agosti mwaka huu.
Lengo la kongamano hilo ni kubuni mikakati na mipango ya pamoja katika tansia ya jiolojia ya madini hususani maendeleo na usimamizi rasilimali hizo kwa manufaa ya ukuaji uchumi na fursa kwa nchi husikak, ambapo jumla ya Mataifa 40 yanatarajia kushiriki katika kongamano hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Madini Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma alisema kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wanasayansi 400 waliofanya tafiti za kisayansi kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Profesa Mruma alisema katika kongamano hilo pia kutakuwapo na uwasilishwaji wa mada na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuhusiana na rasilimali za mafuta, gesi na madini na kwamba Tanzania itatumia kongamano hilo kwa lengo la kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo katika sekta husika.
“Tanzania tuna rasilimali nyingi sana zitokanayo na madini, nishati na gesi kwa mfano tuna mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima pekee mrefu wa volkano uliopo duniani kwa sasa, lakini pia madini ya Tanzanite yaliyopo Arusha yana mwonekano wa kipekee ambao haupo ulimwenguni, na hii ni fursa kwa wanasayansi wa Tanzania kuwaonyesha wenzetu kutoka nje” alisema Profesa Mruma.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kongamano kutoka Taasisi ya YES NETWORK, Stephen Nyagonde alisema kongamano hilo ni la tatu kufanyika duniani, ambapo kwa mara yua kwanza lilifanyika mwaka 2009 Beijing China, baadaye mwaka 2012 nchini Australia.
Akifananua zaidi alisema Katika mkutano huo wanasayansi vijana watapa fursa ya kujadiliana kwa kina na kutoa mapendekezo ya kisayansi ya namna ya dunia kupiga hatua za kimaendeleo na kuboresha maisha ya wakazi wake.
Alisema dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali zitokanazo na athari za jiolojia ikiwemo mafuriko, matetemeko ya ardhi pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo yote kwa pamoja yameleta athari mbalimbali katika maisha ya binadamu na maendeleo ya kiuchumi duniani.
Alisema katika kuelekea mkutano huo, taasisi ya YES NETWORK imepokea jumla ya tafiti 400 ikiwemo tafiti 50 za wanasayansi vijana wa Tanzania, ambazo zote kwa pamoja zinatarajia kuwasilishwa katika kongamano hilo kwa lengo la kubaini changamoto na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta za mafuta, gesi na madini.
Aidha Nyagonde alisema kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa Tanzania, katika kongamano hilo pia kutakuwepo na mada maalum inayohusu somo la hisabati ambalo kwa mujibu wa utafiti somo hilo limekuwa likiwasumbua wanafunzi wengi katika shule za msingi za sekondari nchini.
kongamano linatarajia kuratibiwa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wa Madini Tanzania na chini ya ufadhili wa kampuni ya BG Tanzania kutoka nchini Uingereza.