Quantcast
Channel: Uncategorized – DEWJIBLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Kigoma kumuunga mkono Kafulika

$
0
0

kafulila

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Kigoma kusini, wamesema wapo tayari kuunganishwa na kesi ya Mbunge wao David Kafulila, wakisema kuwa sasa kiburi cha serikali ya Chama cha Mapinduzi sasa inabidi kifike mwisho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika Kazuramimba, Basanza na Uvinza, wananchi hao walioonekana kuwa na hasira, walikataa kuuliza maswali mengi badala yake walikuwa wanaomba kuelekezwa utaratibu ili waweze kuunganishwa na kesi ya Mbunge wao.

“Mimi sina swali, ninataka kujua ni utaratibu gani unaweza kufanywa ili niweze kuunganishwa katika kesi inayomkabili mbunge wetu, kama Mbunge wetu ameitwa tumbili na mwanasheria mkuu wa serikali ya CCM ni dharau ya aina gani kwa sisi tuliomchagua”, alisema mkazi wa Basanza aliyeitwa Abdalla Luvakubandi.

Pamoja na mkazi huyo kuomba mwongozo huo, Wazee kadhaa wa kata ya Kazuramimba,na Uvinza nao walionekana kukerwa wakifika katika mikutano ya Kafulila kwa wingi na kuhoji “yuko wapi anayetaka kumkata kichwa kijana wetu, tunataka kumwona ajue kuwa huku ni Kigoma”. Walisikika.

Kafulila aliyepanga pamoja na viongozi wenzake kufanya mikutano katika mkoa wa Kigoma, alishindwa kufanya mkutano kwenye ngome yake kuu kata ya Nguruka baada ya polisi kumzuia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kwa “usalama wa Mbunge’.

Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Uvinza, Basanza na Kazuramimba, Kafulila amewaambia wananchi wanaotaka kwa hiari yao kuunganishwa na kesi hiyo wajiorodheshe majina ili washitakiwe pamoja.

Wiki iliyopita, Kampuni ya IPTL ilifungua kesi katika mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kumtuhumu Kafulila kwa kuwachafulia jina na kudai fidia ya shilingi Bilioni 310.

Hadi wananchi hao wanaanza kujiorodhesha Kafulila alikuwa amethibitisha kuwa alikuwa hajapata taarifa zozote kiofisi kuhusu yeye kushtakiwa zaidi ya kusikia katika vyombo vya habari.

Kafulila alisema hashangai yeye kushitakiwa, ingawa anajiuliza ni vielelezo gani nchi inahitaji ili kusimama na kusema mchezo mzima wa IPTL ni mchafu. Kwamba IPTL ni mfululizo wa ufisadi tangu ilipoingia na imeendelea kuwa fisadi hadi mwaka 2013 kwenye utoaji wa fedha za akaunti ya Escrow ambazo ni za umma.

“Mwaka 2001, Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kiuwekezaji ya Kimataifa (ICSID), ilitoa hukumu kwamba IPTL ilidanganya kuhusu aina ya mitambo na ikawa ushindi kwa Tanzania, na ndipo ikaamuliwa kushuka gharama za mitambo kutoka dola za Kimarekani milioni 4.2 kwa mwezi mpaka dola za Kimarekani milioni 2.6.

“Kampuni hiyo iliendelea kudanganya kuhusiana na dola milioni 38 wakati hawakuweka kitu, ambapo ukaguzi ulionyesha waliweka dola 50 hali inayoonyesha kuwa nchi inapunjwa zaidi ya dola laki 7.8 kwa mwezi katika malipo hayo.

“Mkataba huu wa IPTL wa miaka 20, maana yake taifa limepoteza na litapoteza zaidi ya sh bilioni 300 kwa uhai wa mkataba, kwamba hivi ni vitu vipo wazi na nyaraka hizi ni za umma, sasa inawezekanaje hawa mafisadi watuibie na watukataze kukasirika?

“Upo ushahidi wa kutosha kwamba mpango mzima ni kupora dola milioni 270, zaidi ya sh bilioni 400, kwa sasa wamepora tayari bilioni 200 kwa kuanzia, ambapo Kampuni ya PAP na IPTL kwa kushirikiana na vigogo wa serikali wamefanikiwa ufisadi huo huku wakivunja sheria na taratibu katika ukwapuaji huo,” alisema.

“Takukuru wanajua, Ofisi ya Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa inajua na wanao ushahidi mpaka majina ya kila aliyehusika na walivyohusika, lakini vyombo vyote vimeshindwa kupeleka wahusika mahakamani na kuacha mkataba wa IPTL unaendelea kuitesa nchi yetu kwa wao kulinda ufisadi,” alisema.

Alisema kuwa ndiyo maana alitaka Kamati Teule ya Bunge ifanyie kazi jambo hilo au kampuni za kimataifa za ukaguzi kama ilivyokuwa EPA, kwani vyombo vya hapa nchini havina nguvu ya kutosha katika hilo.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 5755

Trending Articles