Jaji mstaafu Mark Bomani.
Na Mwandishi wetu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji mstaafu Mark Bomani, amesema Tanzania haitapata Katiba mpya hivi sasa huku akionya kwamba, amani ya nchi itavunjika iwapo jambo hilo litalazimishwa.
Kauli ya mkongwe huyo wa sheria, imekuja wakati tayari wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, wamegawanyika pande mbili, wapo wanaotaka serikali mbili na wengine wanaosisitiza serikali tatu.
Mgawanyiko huo, uliibuka wakati wa kujadili muundo wa serikali, ambako wajumbe kutoka vyama vya upinzani waliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakitaka serikali tatu huku wale wanaotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakisisitiza mbili.
Baada ya kususia vikao vya bunge hilo, viongozi wa Ukawa walizunguka maeneo mbalimbali nchini kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni, huku wajumbe wanaotoka CCM waliyounda kundi la Tanzania Kwanza, nao wakifanya hivyo.
Jaji Bomani alisema, kwa hali ilivyo sasa, ipo siku wajumbe wa Bunge la Katiba watapigana ngumi iwapo watarudi na kuendeleza ubishi wa muundo wa serikali, japo haombei litokee hilo.
“Bunge la Katiba linakwenda kukutana mwezi ujao (Agosti), nina wasiwasi halitafika muafaka… kama litafanikiwa mimi nitasema Inshaallah,” alisema jaji huyo mtaalam wa sheria na katiba.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, alitumia fursa hiyo kuwaomba Ukawa kurejea bungeni na kujadili masuala mengine muhimu yaliyoainishwa kwenye rasimu ya pili ya tume ya Jaji Warioba.
Jaji Bomani ambaye anatajwa kutengeneza katiba ya Namibia mwaka 1990 na ile ya Burundi mwaka 2000, aliwashauri wajumbe wa Ukawa kuliweka kando suala la muundo wa serikali linalowafanya wakose muafaka hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Kwa uzoefu wangu, Katiba ni kitu kitakatifu, lazima kiungwe mkono na idadi kubwa ya wananchi… ubishi uliopo unaweza kutishia uhai wa muungano wetu, wazanzibari ni kiungo muhimu licha ya ukweli kwamba, wakati wanaungana ridhaa ya watanganyika haikupatikana.
“Kwa maoni yangu naunga mkono maoni ya tume ya Jaji Warioba na hakuna sababu ya kubishana, tuweke kando kidogo mjadala huu wa idadi ya serikali, wajumbe wajadili mambo mengine muhimu pia kwa mustakabali wa taifa letu.
“Zipo athari za kiuchumi iwapo mjadala huu utachukua muda mrefu… pesa nyingi za umma zimetumika na zitatumika bila kupata muafaka, zaidi ya sh bilioni 60 zimetumika kuwalipa wajumbe wa bunge la katiba na tayari tume ya Jaji Warioba ilitumia mabilioni ya shilingi pia.
“…Hapa panaweza kuwa na msalahi binafsi, lazima tuwe makini, mjadala wa idadi ya serikali uzungumzwe baada ya uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza Jaji Bomani aliyebainisha kwamba, kupata Katiba mpya sio jambo la haraka haraka.
Kuhusu mustakabali wa taifa, jaji huyo alisema, serikali imeshindwa kupambana na maadui watatu waliokuwepo kabla na baada ya uhuru, ambao Mwalimu Nyerere alianza kupambana nao alipoingia madarakani.
“Muda mfupi baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere aliwataka Watanganyika kupambana na adui ujinga, maradhi na umaskini, ambao hadi sasa bado wapo, nadhani tungejikita kutokomeza maadui hawa.
“Mafanikio yaliyopatikana katika kupigana na maadui hawa hadi leo hayaridhishi… hatujafuta ujinga, maradhi ya kawaida kama malaria tumeshindwa kuyamaliza, umaskini umekithiri unatesa idadi kubwa ya watanzania.