Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima akifungua rasmi mafunzo hayo ya siku pili kwa waandishi wa habari za kodi nchini jijini Dar es Salaam.
Na Damas Makangale, MOblog Tanzania
SERIKALI imewataka waandishi wa habari nchini kuelimisha Watanzania umuhimu wa kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kuwaeleza madhara ya kukwepa kulipa kodi hiyo kwa taifa.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima, wakati akifungua mafunzo ya siku pili ya kodi kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Kodi Tanzania (TAWNET) Mafunzo hayo yalifanyika Chuo cha kodi (ITA).
Amesema kuwa kodi ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Serikali ambayo yanatumika kuendesha uchumi wan chi husika na uhai wa serikali yeyote ni kutegemea kodi zinazolipwa na wananchi.
Malima alifafanua kuwa kodi hizo husaidia kulipa wafanyakazi wa umma, kujenga miundo mbinu kama barabara, reli viwanja vya ndege, mashule, hospitali na kuendesha shughuli za kila siku za nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Kodi Tanzania (TAWNET), Bw Judica Tarimo akizungumza na wanachama wa mtandao wakati uzinduzi rasmi ya mafunzo hayo ya siku pili kushoto kwake ni Mwakilishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Saleh Mshoro, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima na mwisho kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Mlipa Kodi, Bw Richard Kayombo.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuhakikisha inakusanya kodi kutoka vyanzo mbalimbali na hilo linafanyika kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), ambayo imeanzishwa na sheria ya Bunge namba 11 ya mwaka 1995 na kuanza shughuli zake rasmi Julai mwaka 1996.
“Ndiyo chombo kilichopewa dhamana ya kuratibu na kukusanya kodi mbalimbali za serikali Kuu. TRA imekuwa ikifanya kazi nzuri katika ukusanyaji wa mapato na hii inathibitishwa na ongezeko la makusanyo kila mwaka,” amesema Malima na kuongeza;
“Sote tunafahamu kuwa, mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha jambo lolote lile. TRA imeweza kushirikiana vyema na vyombo vya habari kusambaza elimu ya kodi kwa wananchi jambo ambalo limepelekea kuongeza kiasi cha makusanyo kila mwaka,”amesema Malima.
Hata hivyo, amesema uelewa wa wanahabari wengi kuhusiana na masuala ya kodi bado si wa kuridhisha hivyo kuanzishwa kwa TAWNET kutasaidia kukuza uelewa kwa waandishi wa habari.
“Kuundwa kwa mtanda huo ni chachu muhimu ya kwani utaweka pamoja waandishi wa habari na kutumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ya elimu ya kodi na hivyo kuweza kuupa umma habari za uhakika na zenye ubora,” amesema.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Bw Joseph Chikongoye, akizungumza kwa kumkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mhe. Adam Malima kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku pili kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Kodi Tanzania.
”Napenda niwapongeze TAWNET kwa kuja na wazo hili jema ambalo linalenga kuisadia nchi kwa kutumia mtandao wenu kuuhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kodi ikiwa ni pamoja na kuwaeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe,”alifafanua Malima..
“Kalamu ina nguvu na ni matumaini yangu kama mtaitumia vizuri kadiri ya malengo yenu ni wazi kuwa mabadiliko chanya yatapatikana,”aliongeza.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo,Judica Tarimo amesema kuwa anatambua umuhimu wa vyombo vya habari kuandika habari za kodi na kutokana na umuhimu wake iliona haja ya kuwa na waandishi waandamizi ambao watakuwa na uelewa wa kuandika habari hizo.
Amesema ni kweli waandishi wa habari wamekuwa wakiandika habari za kodi lakini kuna makosa mbalimbali ambayo yamekuwa yakijitokeza na kwa kuliona hilo mtandao huo umekuja kuwaunganisha waandishi wa habari za kodi kupata elimu ambayo itawasaidia katika kufanya kazi yao kwa umakini na ueledi mkubwa.
Pia alitoa shukrani zake kwa TRA kwa kuwa sehemu ya kufanikisha mafunzo hayo kwa waandishi wa habari na kusisitiza imani yake ni kwamba waandishi hao watakuwa na uelewa mpana wa masuala ya kodi.