Wabunge nchini Urusi wameidhinisha mswada unaoruhusu hukumu ya vifungo vya jela vya hadi miaka mitatu kwa kosa la kuwaudhi waumini wa kidini.
Mswada huo ulianzishwa mwaka jana baada ya wanachama wa kundi la wanamuziki la Pussy Riot nchini humo kufanya onyesho ambalo halikutarajiwa kumkejeli Rais Vladimir Putin katika kanisa moja mjini Moscow.
Mswada mwingine unaopiga marufuku propaganda ya mahusiano ya jinsia moja yanayolenga watu wa umri mdogo pia umepitishwa na bunge hilo.
Waandamanaji wanaopinga miswada hiyo walifanya shindano la kubusiana nje ya Ikulu ya Rais kabla ya kupitishwa kwa miswada hiyo lakini walizidiwa nguvu na polisi na kundi jingine lililokuwa likiunga mkono kupitishwa kwa miswada hiyo.-DW.