Serikali ya Uingereza kwa mara ya kwanza imetambua mateso na ukandamizaji vilivyofanywa na maafisa wake wa kikoloni katika operesheni za kuzima uasi wa Mau Mau nchini Kenya mnamo miaka ya 1950.
Hata hivyo nchi hiyo imesema haiwajibiki kutokana na vitendo hivyo vilivyofanywa na watawala wa kikoloni, na badala yake imekubali kulipa fidia ya kiasi cha euro milioni 23 kwa wazee takribani 5000 nchini Kenya ambao waliathiriwa na vitendo hivyo.
Kila mmoja wa wazee hao atapata kiasi cha Euro 4,700.
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague ameomba radhi kwa niaba ya serikali yake, kwa kile alichokiita uvunjaji wa haki za binadamu uliovuruga mchakato wa kupigania uhuru wa Kenya.
Amesema Uingereza inavilaani vitendo hivyo kwa nguvu zote.