Kweli Urais hauna ubia wala muda ama sehemu ya kuchapa kazi. Wakati wowote na mahali popote ni sehemu ya kazi, kama inavyoonekana hapa ambako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametulia ndani ya ndege akisafiri kutoka Dar es salaam kuelekea Dodoma huku akiifanyia kazi hotuba yake ambayo ataitoa katika Kikao cha Bunge Maalum la Katiba, leo Ijumaa, Machi 21, 2014.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amealikwa kuwa mgeni rasmi na kuhutubia Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa Kanuni 7(1)g na Kanuni 75(1) la ya Kanuni za Bunge Maalum. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jana, Alhamisi, Machi 20, 2014, amewasili mjini Dodoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambako miongoni mwa mambo mengine atakuwa Mgeni Rasmi na atahutubia Bunge Maalum la Katiba leo, Ijumaa, Machi 21, 2014.
Muda mfupi baada ya kuwa amewasili na kulakiwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kwenye Uwanja wa Ndege wa Mjini Dodoma, Rais Kikwete ameendesha Kikao cha Baraza la Mawaziri lake kwenye Ukumbi wa TAMISEMI ikiwa ni shughuli yake ya kwanza katika ziara hiyo fupi ya Mkoa wa Dodoma.
Leo, Ijumaa, Rais Kikwete atakuwa mgeni rasmi na atahutubia Bunge Maalum la Katiba kutokana na mwaliko wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mheshimiwa Samuel J. Sitta ambaye alimwalika Rais Kikwete kwa barua yake ya Machi 15, mwaka huu, ambayo ilijibiwa Machi 18, mwaka huu, kwa Rais Kikwete kukubali mwaliko huo.
Mwaliko huo wa Mheshimiwa Sitta kwa Rais Kikwete umetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1) (g) na Kanuni 75 (1) ya Kanuni za Bunge Maalum ambazo zinampa Mwenyekiti wa Bunge Maalum madaraka ya kumwalika Mgeni Rasmi aweze kuhutubia Bunge Maalum.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
20 Machi, 2013