Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee (KJF), Hatim Karimjee (kushoto), akikabidhi begi kama ishara ya kutoa ufadhili kwa Dk. Rehema Laiti kwa ajili ya kusoma shahada ya pili ya Udaktari bingwa wa magonjwa ya saratani ya watoto katika hafla iliyofanyika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Kulia ni Dk Shakilu Kayungo mmoja wa madaktari ambaye pia amepoke ufadhili huo na wa pili kushoto ni Dk .Trish Scanlan mratibu wa kozi hiyo.
Na Damas Makangale, MOblog Tanzania
Taasisi ya Karimjee Jivanjee (KJF) imetoa shilingi milioni 70 za kitanzania kudhamini masomo ya shahada ya pili ya magonjwa ya kansa kwa watoto kwa madaktari wawili wa kitanzania watakao soma Chuo kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS).
Akizungumza wakati wa kukabidhi udhamini huo katika wodi ya kansa ya watoto jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa KJF, Ndugu Hatim Karimjee amesema kwamba dk Rehema Laiti na dk Shakilu Kayungo wanakuwa watanzania wa kwanza kupata udhamini wa masomo ya shahada ya pili ya udaktari wa magonjwa ya kansa kwa watoto nchini.
Amesema Tanzania haina madaktari bingwa wa kansa ya watoto wenye shahada ya pili kwa hiyo watakuwa madaktari wa kwanza kupata shahada hiyo kwa mara ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS)
“Wao wamepokea msaada wa udhamini wa masomo kutoka taasisi yetu na fedha zitatoka katika taasisi hii KJF kwa miaka miwili ikiwa ni pamoja na miezi mitatu ya mafunzo kwa vitendo katika moja ya hospitali za kimataifa nchini Ireland,”
“Gharama za masomo zinazotolewa na Karimjee Jivanjee Foundation ni fedha za kitanzania shilingi milioni 70 kwa ufadhiliwa wa madaktari wawili hao, ” amesema.
Amesema Tanzania kama nchi imekuwa ikiahidi kupitia Mpango wa kupambana na saratani kitaifa kwa kutoa huduma hiyo bure kwa wagonjwa wote wa kansa kwa watoto na watu wazima kwa kushirikiana na taasisi za kujitolea za magonjwa ya kansa kama (Rotary Clubs).
Ndugu Karimjee alibainisha kuwa matibabu ya kansa ni bure kutolewa na taasisi ya kansa nchini na wanahudumia takribani wagonjwa 400 hadi 500 Kila mwaka.
Amesema kupitia Shirika Lisilo la Kiserikali la (Cross fire) kutoka Ireland ambao wamefanya kazi hapa nchini tangu 2008 walisaidia kujenga wodi mpya ya watoto wenye magonjwa ya kansa kwa gharama ya dola za kimarekani 700,000.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa kansa za watoto kutoka Ireland, Dk Trish Scnlan amesema kuwa Mpango wa mafunzo ya shahada ya pili kwa madaktari wa magonjwa ya kansa kwa watoto unatokana na ushirikiano kati ya wizara ya afya, chuo kikuu cha muhimbili, hospitali ya muhimbili na wafadhili kadhaa wakiwemo taasisi ya karimjee.
Dk. Scanlan aliongeza kwamba kwa miezi mitatu ya mafunzo madaktari hao watakuwa wakijifunza kwa vitendo kutoka hospitali mbalimbali za ulaya na kupata uzoefu kwa wenzao jinsi ya kuhudumia na kutibu watoto wenye kansa mbalimbali.
“Msingi wa kutoa mafunzo haya ni kutoa uwezo kwa madaktari wa ndani na uanzishwaji wa kliniki za watoto katika kurahisisha tiba ya kansa hapa nchini,” alisisitiza
Alifafanua kwamba Tanzania kwa sasa haina wataalamu mabingwa wa magonjwa ya kansa kwa watoto zaidi ya Dk Trish SCANLAN na Dk Rehema Laiti, Shakilu Kayungo ambao wanatarajiwa kuwa madaktari wa kwanza wenye shahada ya pili kwenye magonjwa ya kansa kwa watoto.