Meya wa Jimbo la California Mstahiki Osby Davis akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kuzungumza naye akiuongoza Ujumbe wa Viongozi, Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Jimbo hilo kuangalia maeneo ya uwekezaji Nchini Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Jimbo la California unaoongozwa na Meya wa Jimbo hilo Mstahiki Osby Davis aliyepo kulia yake.
Balozi Seif akiwa katika picha ya Pamoja na Ujumbe wa Jimbo la California Nchini Marekani uliopo nchini kwa ziara ya siku tatu kuangalia fursa za uwekezaji Vitega Uchumi.
Kulia kwa Balozi Seif ni Meya wa Jimbo la California Mstahiki Osby Davis na Mjumbe wa Sakramento ya Jimbo hilo Bwana Shabir Jiwa.Kushoto kwaa Balozi Seif ni Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar ambaye ndie mwenyeji wa Ujumbe huo Bwana Ali Aboud pamoja na Mjumbe wa Sakramento ya Jimbo hilo Bibi Wanjiru Wanjiru.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Juhudi zilizochukuliwa na Kampuni ya ASB Holdings za ujenzi wa Hoteli ya Daraja la Saba Shangani uliozingatia mpango wa Umoja wa Mtaifa ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe. Kulia kwa Balozi ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza.
Balozi Seif akiangalia mandhari nzuri wa Bahari ya Hindi akiwa juu ya Hoteli ya Daraja la Saba iliyopo Shangani Mjini Zanzibar wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli hiyo.
Moja kati ya vyumba vilivyomo ndani ya Hoteli ya Daraja la Saba iliyopo Shangani Mjini Zanzibar ambayo inaendelea na ujenzi wake ikiwa katika hatua za mwisho mwisho.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Serikali kwa kushirikiana na Taasisi, Mashirika na Jumuiya zinazojitegemea zina wajibu wa kuwajengea uwezo wa Kitaaluma na Uwezeshaji wananchi wenye kipato cha chini ili kupunguza mfumo tegemezi unaonekana kuathiri Mataifa mengi hasa yale yanayojikwamua kiuchumi Duniani.
Kauli hiyo imetolewa na Meya wa Jimbo la California Nchini Marekani Mstahiki Osby Davis wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mstahiki Meya huyo wa Jimbo la California Bwana Osby Davis alisema mpango huo ukizingatiwa vyema na pande hizo husika unaweza kwa kiasi kikubwa kusaidia kujenga jamii itakayojiamini katika kusimamia masuala yanayowahusu kimaisha.
Alisema katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha uchumi wake pamoja na kupunguza ukali wa maisha kwa wananachi wake Uongozi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na Taasisi za uwekezaji upo nchini kuangalia maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kusaidiana na Serikali katika uwekezaji.
Alisema kwamba wapo wafanyabiashara, wawekezaji na hata Makampuni na Taasisi zilizokwishaonyesha nia ya kutaka kutumia fursa iliyotolewa na Zanzibar katika suala zima la uwekezaji Vitega uchumi mbali mbali.
Akitoa shukrani zake kwa uamuzi wa Ujumbe huo wa Viongozi na Wawekezaji wa Jimbo la California Nchini Marekani kutembelea Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Sekta ya Utalii Nchini bado ina fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinaweza kusaidia pato la Taifa.
Balozi Seif alisema juhudi kubwa tayari zimeshachukuliwa na Serikali Kuu katika kuimarisha miundo mbinu ya Mawasiliano, Bara bara pamoja na Huduma za Umeme na Maji safi ili kuwajengea mazingira rahisi wawekezaji wa Sekta ya Utalii watakaoamua kuitumia fursa hiyo.
Ujumbe huo wa Viongozi, Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jimbo la California Nchini Marekani ambao ulianzia ziara Tanzania Bara ulikuwepo Zanzibar tokea Tarehe 27 Mwezi uliopita.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara fupi ya kukagua ujenzi wa Hoteli Mpya ya Daraja la Saba { Grand Hayert } inayojengwa katika eneo lililokuwa Starehe Club ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Ujenzi wa Hoteli hilo inayomilikiwa na Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s unafanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ya CRJ.
Kampuni hiyo ya ASB Holding’s katika ujenzi wake huo imechukuwa hatua za matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO } juu ya kuendeleza hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika makubaliano ya Hifadhi ya Kimataifa.
Ujenzi wa Ukuta Maalum wa mita tatu kama yalivyo majengo mengine ya Mji Mkongwe yaliyo pembezoni mwa Bahari unazingatiwa kwenye Hoteli hiyo ili kunusuru athari yoyote ya Maji, Mazingira au matukio ya Dhoruba yanapotokea wakati wowote.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Issa Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba jengo lililokuwa Mambo msiige ambalo limeambatana na ujenzi huo linafanyiwa matengenezo makubwa kwa kutumia chokaa ili kulinda uasili wake.
Nd. Sarboko alisema matumizi ya saruji katika majengo ya asili ndani ya Mji Mkongwe yaliyojengwa kwa chokaa na udongo mbali ya kuharibu mfumo wake wa kihistoria lakini pia unaondosha ubadhubuti wa majengo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza uongozi wa Hoteli hiyo kwa juhudi zake za kuwekeza kitega uchumi kitakachosaidia kunyanyua sekta ya Utalii ambayo hivi sasa imepewa kipaumbele na Serikali.
Uongozi wa Hoteli hiyo ulimuhakikishia Balozi Seif kwamba ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika rasmi mwezi Agosti mwaka huu na ulilazimika kuchelewa kutokana na baadhi ya vifaa vingi vya ujenzi wake kuchelewa kufika Nchini kwa wakati uliopangwa.
Jengo la Hoteli hiyo ya Daraja la Saba litakalokuwa na ghorofa Tatu unatarajiwa kutoa ajira za wafanyakazi wazalendo kati ya sitini na mia moja wakati litakapoanza kutoa huduma zake.
Othman Khamis Ame-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar