Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassan Dharamsi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maendeleo ya Jimbo lake tokea alipochaguliwa kuwa mwakilishi Mwezi Februari mwaka 2012 katika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar, kushoto Afisa mwandamizi wa Idara ya Habari maelezo Zanzibar Ramadhan Ali.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali wakimsikiliza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassan Dharamsi (hayupo pichani) katika Hoteli ya Grand Palace Malindi alipokuwa akieleza mafanikio aliyopata tokea aliposhinda uchaguzi wa Jimbo lake mwaka 2012.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Muhamedraza Hassan Dharamsi akiwaonyesha waandishi wa habari masuala aliyoyapa kipaumbele katika uongozi wake ndani ya Jimbo hilo ikiwemo elimu katika mkutano uliofanyika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Salum Vuai akimuuliza swali mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassan Dharamsi katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
Na Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassan Dharamsi amemuomba Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Muhammed Shein kuanzisha utaratibu wa kuwafanyia tathmini viongozi wa majimbo juu ya utekelezaji wa majukumu yao kama anavyofanya kwa viongozi wa Taasisi za Serikali ili kufahamu utekelezaji wa majukumu yao kwa wananchi.
Mohamedraza amesema uamuzi wa Dk. Shein kuwaita watendaji wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kila robo ya mwaka (bango kitita) umesaidia sana kuamsha ari ya viongozi kutekelezaji wajibu wao kwa taifa.
Ushauri huo ameutoa leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika Hoteli ya Grand Palace Malindi kuelezezea mafanikio yaliyofikiwa na jimbo la Uzini tokea aliposhinda uchanguzi mdogo wa Jimbo hilo mwaka 2012.
Amesema wakati wagombea katika nafasi mbali mbali wanapoomba kura kutoka kwa wananchi hutoa ahadi nyingi ambazo watazitekeleza iwapo watashinda lakini baada ya kuopata ushindi viongozi hao huwadharau wapiga kura zao.
“Mh. Rais naomba suala la Bango kitita lisiishie kwa viongozi wa Serikali pekee na sasa lipelekwe kwa viongozi wa majimbo kuwapima utekelezaji wa ahadi walizozitoa kwa wananchi,” alisisitiza Mwakilishi huyo.
Amesema iwapo viongozi wataweza kutekeleza ahadi wanazotoa kwa wananchi wao hakuna sababu ya kutoleta maendeleo katika majimbo jambo ambalo litawafanya wananchi kuwa na ari, upendo na kuwa karibu na viongozi wao.
Ameahidi kuwa ataendelea kuwatumikia wananchi wa Uzini kwa hali na mali katika kufanikisha ilani ya CCM na tayari ametekeleza ahadi zake kwa asilimia mia moja licha ya changamoto nyingi anazokabiliana nazo.
Ameongeza kuwa matatizo mengi yaliyokuwa yakilikabili Jimbo hilo ikiwemo miundo mbinu ya barabara, maji safi na salama na mitaji kwa wafanyabiashara ndogo ndogo limepungua.
“Kazi kubwa iliyopo mbele yangu kwa sasa nikishirikiana na viongozi wengine wa Jimbo ni kupunguza wimbi kubwa la vijana wanaoshindwa kuendelea na masomo kutokana na umaskini wa wazazi wao kwa kuwapeleka katika vituo vya mafunzo ya amali kwa gharama zangu” aliahidi Mohamedraza.
Hata hivyo ameomba mashirikiano zaidi katika kupunguza tatizo la umaskini na kuwaletea wananchi maendeleo bila ya kujali itikadi za kisiasa na kuwashauri viongozi kuacha malumbano ambayo hayasaidii kuwakwamua wananchi.
Akizungumzia rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyowasilishwa hivi karibuni, Muhamedraza amesema ataendelea kuunga mkono msimamo wa Chama cha Mapinduzi wa Serikali mbili lakini zenye hadhi sawa kwani zilizoungana ni nchi mbili zilizokuwa na mamlaka kamili kabla ya kuungana.
Muhamedraza Hassan Dharamsi lishinda uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini baada ya kufariki aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Maalim Mussa Khamis Silima kutokana na ajali ya gari Mkoani Dododma mwishoni mwa mwaka 2011.
Wakati wa kampeni zake kwa wananchi mwakilishi huyo aliahdi kutumia mshahara wake na maposho mengine atakayopata katika kupeleka maendeleo ndani ya Jimbo la Uzini.