Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumamosi, Januari 11, 2014, amepokea hati za utambulisho za Balozi mpya wa Comoro katika Tanzania, Mheshimiwa Ahamed El Badaoui Mohamed Fakih.
Katika sherehe fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Mheshimiwa Fakih wamefanya mazungumzo mafupi kuhusu hali ya uhusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo jirani ya Comoro.
Rais Kikwete amemkumbusha Mheshimiwa Fakih uhusiano wa karne nyingi kati ya wananchi wa Tanzania na Comoro, uhusiano ambao umeimarishwa na mahusiano kati ya Serikali za nchi hizo mbili marafiki na majirani.
Rais Kikwete amesema kuwa matokeo ya uhusiano huo wa karne nyingi ni kuwapo kwa Watanzania wengi wenye asili ya Comoro hapa nchini.
Naye Mheshimiwa Fakih, ambaye anakuwa balozi wa kwanza wa Comoro katika Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili, amemshukuru Rais Kikwete na Tanzania kwa kushiriki katika ukombozi wa Kisiwa cha Anjuan, mojawapo ya Visiwa vya Comoro kutoka kwenye uasi wa Kanali M. Bakari.
Aidha, Balozi huyo amempa Rais Kikwete salamu za rambirambi kufuatia kifo cha askari mmoja wa Tanzania alipoteza maisha kwenye operesheni hiyo ya kukomboa Kisiwa hicho iliyosimamiwa na Umoja wa Afrika (AU).